WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma nchini ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Waziri Kikwete amesema hayo leo Mei 21, 2026 wakati akishiriki ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Ngurdoto, Arusha.
Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emanuel Nchimbi, na umehusisha zaidi ya wajumbe 5,050 kutoka Serikali Kuu, halmashauri na taasisi mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri Kikwete ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha ustawi wa watumishi wa umma, ikiwemo kupandisha madaraja, kubadili miundo na vyeo pamoja na kulipa madeni ya mishahara.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza maboresho hayo kila panapopatikana nafasi ya kibajeti ili kuhakikisha watumishi wananufaika na matunda ya nchi yao.
Aidha, amesema Serikali pia imejipanga kuongeza uangalizi kwa Waandishi Waendesha Ofisi (Masekretari) ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Katika mkutano huo, Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi amewahimiza wajumbe wa TAPSEA kuzingatia haki, mshikamano na uadilifu wakati wa uchaguzi wa viongozi wapya wa chama hicho, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda mwelekeo na umoja wa chama.




Comments
Post a Comment