SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza fursa mbalimbali kwa wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Sita, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza vipaji na kukuza wataalamu wa baadaye nchini.
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati akiongea na Waandishi wa Habari leo Mei 4,2026 katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma, amesema kuwa wanafunzi watakaofaulu vizuri watapata nafasi za kujiunga na vyuo vikuu kupitia mifumo ya kitaaluma pamoja na kuzingatiwa katika utoaji wa mikopo kupitia HESLB.
Aidha, Prof. Mkenda Amesema Serikali kupitia Samia Scholarship itaendelea kufadhili wanafunzi bora wa sayansi kwa asilimia 100 katika vyuo vya ndani, hususan katika fani za Hisabati, TEHAMA, Sayansi Asilia, Uhandisi na Tiba.
Kwa wanafunzi wa sayansi wenye ufaulu wa juu zaidi, watachaguliwa kwa mafunzo maalum katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela (NM-AIST) Arusha kabla ya kupelekwa kuendelea na masomo nje ya nchi katika vyuo vikuu mbalimbali.
Pia Serikali imesisitiza kuwa lengo ni kuandaa wataalamu wa sayansi na teknolojia kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended unaojumuisha pia Artificial Intelligence na Data Science.
Wanafunzi wote wanahimizwa kufanya bidii, kwani ufaulu mzuri ni mlango wa fursa kubwa za elimu na maendeleo ya taifa.


Comments
Post a Comment