Mbunge wa zamani wa Jimbo la Butiama Mhe. Jumanne Abdallah Sagini Kwa kushirikiana Taasisi ya ITTIFAK International kutoka nchini Uturuki amechinja Ng'ombe 400 na Kondoo 1000 na kugawanywa kwenye vitongoji 370 na taasisi zote za umma na binafsi zilizopo katika Wilaya ya Butiama ikiwemo baadhi ya misikiti Wilaya ya Musoma mkoani Mara kwa ajili ya kitoweo kwa wananchi kipindi hiki cha kusherehekea Sikukuu ya Eid Al-Adha.
Zoezi hilo la Sadaka limefanyika leo Mei 27, 2026 nyumbani kwake Kijiji cha Kiabakari, Kata ya Kukirango katika Wilaya ya Butiama kama sehemu ya kuimarika kiimani na ukarimu na mshikamano na upendo.
Kwa upande wake Sheikh wa Kata ya Mugango Musoma Vijijini Mwabadi Yusuph Chogero ameeleza kuwa kwa kipindi hiki Sagini amepanua wigo zaidi kwani Sadaka hiyo imewafikia hadi Misikiti Saba iliyopo Musoma Vijijini, huku Sheikh wa Kata ya Kukirango Juma Maharage amesema imekuwa ni desturi ya Sagini kuwaalika wananchi mbalimbali katika kushiriki kitoweo kwa pamoja.
Baadhi ya Taasisi zilizofikiwa na kitoweo hiko ni Shule ya Sekondari ya Kiagata, Bumangi, Chief Ihunyo, Chief Wanzagi, Mkono, Shule ya mahitaji maalumu Kiabakari, Chuo cha Victoria Nyabange, Musoma Utalii, Hope for Girls and Women Tanzania, Magereza na VETA Butiama.
“Ni nadra sana kuona kiongozi mwenye moyo wa kujitolea kwa kiwango hiki. Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumpa afya na baraka,” mmoja wa wakazi wa Butiama amesema.
Aidha zoezi hilo ni muendelezo wa majitoleo anayofanya Sagini katika jamii kila mwaka ambapo sio tu kwa waislamu pia kwa wakristo ameendelea kuwagusa katika kusaidia ujenzi, kushiriki sikukuu zao na utoaji wa zaka mbalimbali, lengo kubwa ni kuifanya jamii kuwa pamoja na kudumisha mshikamano uliojengwa toka zamani.









Comments
Post a Comment