Rais Samia arejea Nchini kutoka Uganda

GEORGE MARATO TV
0


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amerejea nchini baada ya kuhudhuria Sherehe za Uapisho wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Jijini Kampala, tarehe 12 Mei, 2026.

Akiwa nchini Uganda mh Rais Samia Suluhu Hassan, amehudhuria sherehe za uapisho wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, zilizofanyika jijini Kampala, Uganda.






Rais Museveni ameapishwa kuiongoza Uganda kwa muhula mwingine baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 15 Januari, 2026.

Ushiriki wa Rais Dkt. Samia ni kielelezo cha kuendeleza uhusiano wa kindugu na kihistoria kati ya Tanzania na Uganda, unaojengwa katika misingi ya umoja, mshikamano, ujirani mwema na ushirikiano wa kikanda, kwa maslahi ya pamoja ya wananchi wa pande zote mbili.

Tanzania na Uganda ni washirika wa karibu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakiendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja za diplomasia, biashara, uwekezaji, nishati, uchukuzi, miundombinu, kilimo, viwanda, uhamiaji na miradi ya kimkakati ya kikanda.

Katika biashara, nchi hizo zimeendelea kuboresha mifumo ya uwezeshaji biashara, uongezaji wa thamani za bidhaa na kushirikiana katika kutatua changamoto zilizopo ikiwemo vikwazo visivyo vya kikodi. Hatua hii inalenga kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma ndani ya ukanda kupitia ushoroba wa kati.

Katika uwekezaji, sekta binafsi za Tanzania na Uganda zimeendelea kuwa sehemu muhimu ya kukuza mitaji, ajira na uzalishaji, hususan katika viwanda, usafirishaji, kilimo, utalii na huduma.

Kupitia Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) ya ushirikiano, nchi zote mbili zimeendelea kuweka mikakati thabiti ya kutekeleza miradi ya pamoja, ikiwemo Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), reli ya kisasa (SGR) kutoka Isaka, Lusahunga, Murongo/Kikagati hadi Mpondwa nchini Uganda; bomba la gesi asilia, bomba la mafuta yaliyosafishwa, na ujenzi wa barabara.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Samia amerejea nchini leo jioni Mei 12,2026 huku Biashara kati ya Tanzania na Uganda imeendelea kukua, ambapo mauzo ya Tanzania kwenda nchini Uganda yalifikia takribani Dola za Marekani milioni 134.7 mwaka 2025, huku mauzo ya Uganda kwa Tanzania yakifikia takribani Dola za Marekani milioni 88.2.

Kati ya mwaka 2014 na 2024, Tanzania ilisajili miradi 38 ya uwekezaji kutoka Uganda, yenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 126.49, iliyozalisha fursa 2,911 za ajira.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top