RAIS wa Kenya, William Samoei Ruto, ametoa wito kwa nchi za Afrika Mashariki kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uhuru wa usafiri wa watu, bidhaa na huduma, akisisitiza kuwa mshikamano wa kikanda haupaswi kuzuiliwa na mipaka ya kisiasa.
Akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo Mei 5, 2026, katika hitimisho la ziara yake ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania, Ruto amesema uhalisia wa maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki tayari unaonesha umoja wa dhati.
“Wananchi wetu tayari wameunganishwa kupitia familia, biashara na shughuli za kiuchumi zinazovuka mipaka; ni wajibu wa sera zetu kuendana na hali hiyo,” amesema Ruto.
Amebainisha kuwa kuna maelfu ya wananchi wenye ndugu pande zote za mipaka, huku wafanyabiashara na wajasiriamali wakitegemea usafirishaji rahisi ili kukuza shughuli zao za kiuchumi.
“Hatuwezi kuzungumzia soko la pamoja huku tukidumisha vikwazo vinavyowazuia wananchi na bidhaa zao kusafiri kwa uhuru,” ameongeza.
Akitoa mfano wa umoja wa asili, Ruto ametaja uhamaji wa wanyamapori kati ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na Maasai Mara, akisisitiza kuwa hata maumbile hayazingatii mipaka ya kisiasa.
“Kila mwaka mamilioni ya wanyamapori husafiri bila kujali mipaka,hili linatufundisha nini kuhusu ushirikiano wetu?”.
Aidha, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujifunza kutokana na historia ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo mwaka 1977.
“Changamoto zilizopita zilikuwa za kiutendaji, si za kimsingi zinaweza kuepukika kwa dhamira ya pamoja,” amesema.
Rais pia amesisitiza suala mshikamano na ushirikiano wa karibu kama msingi wa kujenga Afrika Mashariki imara.
“Tunahitaji dhamira ya dhati ili kujenga ukanda wenye umoja unaowanufaisha wananchi wote.”




























Comments
Post a Comment