WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amewatakia kila la kheri wanafunzi wa Kidato cha Sita pamoja na waalimu tarajali wote wanaoanza mitihani yao leo Mei 4,2026.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, jumla ya wanafunzi 165,655 wa Kidato cha Sita wameanza mitihani yao leo, ambayo itaendelea hadi tarehe 15 Mei 2026. Kwa upande wa waalimu tarajali, takribani 14,669 nao wameanza mitihani yao na watahitimisha tarehe 18 Mei 2026.
Akizungumza leo Mei 4,2026 katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma kuhusu zoezi hilo, waziri wa Elimu Sayansi na Teknlojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali inaungana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwapa moyo watahiniwa wote nchini.
“Napenda kuwapongeza sana wanafunzi wa Kidato cha Sita pamoja na waalimu tarajali kwa kufikia hatua hii muhimu ya mitihani. Serikali inawaombea kila la heri, utulivu na mafanikio mema katika kipindi hiki.” Amesema
Aidha, amesisitiza umuhimu wa uadilifu na kufuata taratibu za mitihani, akionya dhidi ya vitendo vya udanganyifu.
“Nawaomba watahiniwa wote wazingatie sheria na kanuni za mitihani. Tumejipanga vizuri kuhakikisha kila mmoja anafanya mitihani kwa haki na usawa. Hatutavumilia kabisa vitendo vya udanganyifu.”
Prof. Mkenda amesema mwenendo wa usimamizi wa mitihani nchini unaendelea kuwa wa kuridhisha, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda uaminifu wa mfumo wa elimu.
Pia amewakumbusha wanafunzi kuwa mitihani hiyo ni mlango muhimu wa fursa za elimu ya juu.“Huu ni wakati wa kujituma na kuamini uwezo wenu. Mafanikio katika mitihani hii yatawafungulia milango ya vyuo vikuu na fursa mbalimbali za kitaaluma ndani na nje ya nchi.” Amesema
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa maendeleo ya Taifa.


Comments
Post a Comment