Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilijadili namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Uingereza katika sekta ya ulinzi na usalama, ikiwemo mafunzo, mapambano dhidi ya ugaidi pamoja na usalama wa majini.
Balozi Marianne Young alisema Tanzania ni mshirika muhimu wa Uingereza kutokana na historia na uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya mataifa hayo mawili, huku akieleza utayari wa serikali ya Uingereza kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo uchumi, utamaduni na maendeleo ya kijamii.
Aidha, Balozi huyo aliipongeza Wizara ya Ulinzi na JKT pamoja na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo na kuendelea kuliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uzalendo.
Kwa upande wake, Waziri Dkt. Rhimo Nyansaho alimshukuru Balozi Marianne Young kwa ziara hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano uliopo pamoja na kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza katika sekta ya ulinzi na usalama.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na maafisa waandamizi kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania.








Comments
Post a Comment