📍Atimiza miaka 41 na kusherehekea kwa aina ya kipekee
📍Aguswa na uchungu wa kuishi bila wazazi
Na MWANDISHI WETU, Muheza
NIMEAMUA kuweka alama ya kumbukumbu ya siku yangu ya kuzaliwa kwa kuamua kuwa mlezi wa watoto 41 wanaoishi katika mazingira magumu.
Watoto hao 41 kama ilivyo miaka aliyoishi duniani, Faraja Kotta mwanasiasa chipukuzi, alisema ameguswa kufanya hivyo kwa sababu maumivu ya kupoteza wazazi akiwa mdogo bado anayahisi hadi leo.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Mei 6 mwaka huu, katika kituo cha Daarul Abideen, kilichopo Mkanyageni wilayani Muheza Faraja alisema sherehe yake hiyo itabaki katika Kumbukumbu ya maisha yake.
Faraja amejitwika jukumu la ulezi kwa watoto hao wanaotoka katika kata 17 za wilaya hiyo, akiahidi kuwasaidia katika huduma za afya kupitia bima, elimu, na mahitaji ya msingi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali watakaoguswa kuungana naye katika jukumu hilo.
" Niliamua kuweka alama ya kumbukumbu ya siku yangu ya kuzaliwa kwa kuamua kuwa mlezi wa watoto hawa 41. Idadi yao ni 41 kama ilivyo miaka niliyoishi duniani" alisema Faraja.
Alisema kuwa aliamua kula chakula cha mchana kwa pamoja na kituo cha Daarul Abideeen, ili pia aweze kutatua baadhi ya changamoto zao ikiwemo kuendelea kuboresha kituo hicho.
*Kilio cha Watoto 1,000 Muheza*
Hafla hiyo imekuja wakati Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Muheza, Kibbah Mwakyusa, alibainisha kuwa zaidi ya watoto 1,000 katika wilaya hiyo wanaishi katika mazingira hatarishi.
Mwakyusa alieleza kuwa idadi hiyo inajumuisha yatima na watoto wenye mahitaji maalum ambao wanakabiliwa na uhaba wa mahitaji ya msingi ambapo wamekuwa wakiyakosa kutokana na kukosa wazazi.
"Mara nyingi tunawafikia baadhi yao, lakini bado wengi wanahitaji msaada zaidi, hasa katika maeneo ya afya na elimu. Kitendo cha Faraja Kotta ni mfano bora wa kuigwa na jamii," alisema Mwakyusa.
*Msaada wa Tenki la Maji*
Mbali na chakula cha pamoja, Faraja ametoa msaada wa tenki la maji kufuatia changamoto ya uhaba wa maji inayokikabili kituo hicho.
Meneja wa kituo cha Daarul Abideen alishukuru msaada huo akisema utasaidia kupunguza adha ya usafiri na uhitaji wa maji safi kwa watoto wanaolelewa hapo.
Faraja, ambaye mwaka jana alishiriki kuwanadi wagombea wa CCM kwenye uchaguzi Mkuu, ametoa wito kwa wazazi kuwathamini watoto na kuwalinda dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaochochewa na mitandao ya kijamii.
Alimalizia kwa kuishukuru Serikali, viongozi wa CCM na UWT kwa kuendelea kumuunga mkono katika harakati zake za kusaidia jamii.








Comments
Post a Comment