OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imezindua matokeo ya tafiti mbili muhimu zilizotajwa kuwa miongoni mwa nyenzo zitakazosaidia Taifa kupanga maendeleo kwa kutumia takwimu sahihi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Tafiti hizo ni Utafiti wa Uwezeshwaji Wanawake na Lishe wa Mwaka wa Kilimo 2023/2024 pamoja na Utafiti wa Mazingira na Jinsia wa mwaka 2025, zilizofanywa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Benki ya Dunia, Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) na UN Women.
Akizindua Tafiti hizo leo Mei 6, 2026 katika Makao Makuu ya ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Tafiti hizo zimefungua ukurasa mpya wa matumizi ya takwimu katika kuibua suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii.
“Hizi ni tafiti za kwanza kufanyika Tanzania, na kwa upande wa Afrika, utafiti wa mazingira na jinsia ni wa pili baada ya Senegal. Hii ni fahari kubwa kwa Taifa letu,” amesema Dkt. Gwajima.
Matokeo ya Tafiti hizo yameonesha kuwa asilimia 26 pekee ya wanawake nchini wanaamini wanawake wanapaswa kuwa na haki ya kufanya maamuzi kuhusu njia za kujikimu kimaisha.
Takwimu hizo pia zimeonesha kuwa asilimia 34 ya wanawake wanaunga mkono haki za wanawake kuhusu ndoa, talaka na kupata watoto, huku asilimia 56 wakipinga aina zote za unyanyasaji dhidi ya wanawake.
Dkt. Gwajima amesema matokeo hayo yanaonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kuweka mazingira yatakayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuzalisha takwimu sahihi na za kuaminika ili kusaidia upangaji wa sera na mipango ya maendeleo.
“Takwimu ni msingi wa maamuzi sahihi. Bila takwimu sahihi, ni vigumu kupanga maendeleo yenye matokeo chanya kwa wananchi,” amesema Dkt. Msengwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Takwimu ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kuhakikisha matokeo ya tafiti hizo yanatumika ipasavyo katika kufanya maamuzi ya maendeleo.
“Takwimu hizi ziwe mwanga wa maamuzi yatakayobadilisha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo yenye usawa,” amesema Makinda.
Dhamira ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni Kutoa takwimu rasmi zilizo bora na huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa kitaifa na kimataiafa kwa ajili ya kupanga mipango na kutoa maamuzi sahihi.




Comments
Post a Comment