*EID AL-ADHA MUHEZA:*
Na Mwandishi Wetu, Muheza
MBUNGE wa Muheza, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), ameshiriki Swalah ya Eid Al-Adha iliyofanyika katika uwanja wa Jitegemee wilayani hapa, na kuwataka waumini wa Kiislamu kudumisha amani.
Swalah hiyo kubwa ya iliongozwa na Sheikh Khatibu, ambaye kabla ya kuanza ibada, aliwasihi Waislamu kufuata kikamilifu mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW) na kuacha kupoteza muda mwingi kwenye mambo yasiyo na msingi.
Sheikh Khatibu aliwakumbusha waumini hao umuhimu wa kufanya ibada za funga zilizowekwa kisheria katika siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah ili kujisogeza karibu na Mwenyezi Mungu.
Akisalimia maelfu ya waumini waliofurika uwanjani hapo, Mhe. Mwinjuma aliwatakia heri ya sikukuu ya Eid na kuwasisitiza kuendelea kuwaombea viongozi wakuu wa nchi kila wanapofanya ibada zao.
"Tunapoendelea kufurahia sikukuu hii ya kuchinja, nawaomba sana ndugu zangu tusiache kuwaombea viongozi wetu wa kitaifa, hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili Mungu aendelee kumpa nguvu ya kuliongoza Taifa letu kwa amani," alisema MwanaFA.
*Ng'ombe 150 Wachinjwa Mzambarauni*
Mara baada ya kukamilika kwa Swalah hiyo, Mbunge huyo alielekea katika Kijiji cha Mzambarauni kilichopo Kata ya Mlingano wilayani hapa, ambapo alishiriki rasmi ibada ya dharura ya kuchinja wanyama.
Katika eneo hilo, Mhe. Mwinjuma alikaribishwa na jumuiya ya wafadhili kutoka nchini Uturuki (Waturuki Kurban) wakishirikiana na Taasisi ya Islamic Help Tawi la Muheza, chini ya msimamizi wao, Bw. Sabri Said.
Mbunge huyo alitoa pongezi za dhati kwa taasisi hiyo kwa kuendesha zoezi hilo kubwa ambalo linakwenda kuwasaidia wapiga kura wake wasio na uwezo kupata kitoweo cha nyama kwa ajili ya kusheherekea sikukuu hiyo na familia zao.
"Nawashukuru sana Islamic Help na washirika wenu. Zoezi hili lina thawabu kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini pia linazisaidia kaya zetu zisizojiweza kupata kitoweo na kushiriki ibada hii ya machinjio kupitia ninyi," alishukuru Mbunge huyo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Islamic Help Wilaya ya Muheza, Bw. Sabri Said, alianika takwimu za mradi huo na kueleza kuwa jumla ya ng'ombe 7,080 wamechinjwa mkoa mzima wa Tanga, ambapo kwa Wilaya ya Muheza pekee zoezi hilo limehusisha uchinjaji wa zaidi ya ng'ombe 150.









Comments
Post a Comment