Na Mwandishi Wetu
SHULE ya St Anne Marie Academy iliyoko Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam mwaka huu inatimiza miaka 25 yenye mafanikio makubwa kwenye utoaji wa elimu bora tangu kuanzishwa kwake.
Tarehe 18 Julai mwaka huu itatimiza miaka 25 ikiwa ni miongoni mwa shule bora nchini ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kwenye matokeo ya kitaaluma kuanzia ngazi ya kata, Wilaya, Mkoa hadi kwenye ngazi ya taifa.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), ambaye pia ni Mkurugenzi Mwanzilishi wa shule hizo Dk Jasson Rweikiza wakati akizungumzia miaka 25 ya kutoa huduma ya elimu.
Dk Rweikiza miongoni mwa mafanikio makubwa ya shule hiyo kwa miaka 25 ni kutoa mwanafunzi bora kitaifa katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani NECTA mwaka 2021.
Alisema licha ya kutoa mwanafunzi bora kitaifa mwaka 2021, shule hiyo imekuwa ikifanikiwa kuingiza wanafunzi wengi kwenye 10 bora kitaifa kwa miaka mingi na imepata pongezi nyingi kitaifa na kimataifa.
“Upekee wa shule yetu ya St Anne Marie Academy ni kuwa na miundombinu bora kama maktaba zenye viyoyozi zilizosheheni vitabu vya kila aina, maabara za kisasa za sayansi zinazowawezesha wanafunzi wa masomo ya sayansi kusoma kwa vitendo,” alisema Dk Rweikiza.
Aidha, alisema St Anne Marie Academy ni shule ya kwanza na ya pekee nchini kuanzisha utaratibu wa kuwasomesha bure hadi kumaliza masomo yao wanafunzi wa shule hiyo wanaofiwa na mzazi anayelipa ada.
“Tumekuwa tukiahidi na kutekeleza kwamba hakuna mwanafunzi atakayefukuzwa shule kwa kukosa ada baada ya kufiwa na mzazi aliyekuwa akilipa ada, kama mwanafunzi yuko darasa la kwanza basi atasoma hadi darasa la saba na kama yuko kidato cha kwanza basi atamaliza kidato cha nne,” ni kauli ya Dk Rweikiza ambayo amekuwa akiitoa mara kwa mara kwenye mahafali shuleni hapo.
Dk Rweikiza alisema matokeo bora ya shule hiyo ni jambo ambalo halijatokea kwa bahati bali ni kutokana na moundombinu bora iliyowekwa ikiwemo bodi ya mitihani ndani ya shule hiyo.
“Ili kuongeza ufanisi wa kitaaluma, kazi ya kutunga mitihani shuleni kwetu St Anne Marie Academy imekuwa ikifanywa na bodi hiyo ya mitihani na walimu wanakuwa na kazi ya kufundisha tu hali ambayo imeongeza ufaulu kwa kiwango kikubwa,” alisema
“Walimu wa St Anne Marie Academy tumewaachia kazi ya kufundisha tu, kazi ya kutunga mitihani ni ya bodi ya mitihani na tangu tuanzishe utaratibu huu tumeona mafanikio makubwa sana ya kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wetu,” alisema Dk Rweikiza.

Comments
Post a Comment