WAZIRI wa Afya Mohamed Mchengerwa ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kupima magonjwa ya afya ya akili, hususan msongo wa mawazo na sonona, akisema changamoto hizo zinaongezeka lakini zinatibika endapo zitagundulika mapema.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma leo Mei 11, 2026, Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya ya akili nchini ili kuwasaidia wananchi kupata matibabu na msaada wa kisaikolojia kwa wakati.
“Nitoe rai kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya kupima magonjwa ya afya ya akili hususan msongo wa mawazo na sonona,” amesema Mchengerwa.
Amesema kati ya Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya watu 254,932 walipatiwa huduma za afya ya akili pamoja na msaada wa kisaikolojia katika vituo vya afya vya msingi nchini, huku upatikanaji wa dawa za afya ya akili ukifikia wastani wa asilimia 75 katika vituo vya kutolea huduma.
Aidha, Serikali imeendelea kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kusaidia kutambua mapema changamoto za afya ya akili na kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Katika kipindi hicho, watu 1,709 walifanyiwa uchunguzi wa sonona ambapo 1,362 walibainika kuwa na changamoto hiyo na wanaendelea kupatiwa matibabu.


