WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Poul Makonda, amesema Serikali imeendelea kupata mafanikio makubwa katika sekta ya michezo nchini, hatua inayodhihirisha ukuaji wa vipaji na kuimarika kwa ushindani wa kimataifa.
Akizungumza leo Mei 4, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo, Makonda amesema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji wa kimkakati pamoja na usimamizi madhubuti wa shughuli za michezo.
Ameeleza kuwa mashindano ya CHAN 2024 yaliyofanyika mwaka 2025 kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda yameacha alama kubwa, huku timu ya Taifa “Taifa Stars” ikionesha ushindani wa hali ya juu kwa kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali.
“Hii ni ishara kuwa soka letu la ndani linazidi kukua na kuimarika,” amesema Makonda.
Amesema kuwa ubora wa maandalizi na usimamizi wa mashindano hayo uliifanya Tanzania kuendelea kuaminiwa kimataifa, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alitunukiwa tuzo ya heshima na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Katika maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, Makonda amesema Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo katika miji ya Dar es Salaam na Arusha, ambapo hatua mbalimbali zimefikiwa ikiwemo ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa Stadium uliokaribia kukamilika pamoja na ujenzi wa viwanja vya mazoezi na uwanja mpya wa Arusha unaoendelea vizuri.
“Ni matarajio yetu kukamilisha miundombinu yote kwa wakati ili Tanzania iwe tayari kwa mashindano haya makubwa,” amesisitiza.
Aidha, amesema Serikali imeweka mkazo mkubwa kuhakikisha maandalizi hayo yanafanikiwa, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha fedha za kutosha kugharamia mchakato huo.
“Hii inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuendeleza michezo na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa,” ameeleza.
Makonda pia amewapongeza wanamichezo wa Tanzania wanaoendelea kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, akiwemo Alphonce Felix Simbu kwa mafanikio yake ya medali ya dhahabu duniani.
“Mafanikio ya wanamichezo wetu ni matokeo ya uwekezaji na juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali,” amesema.
Ameonheza kuwa mafanikio ya timu za taifa pamoja na ushiriki wa Tanzania katika mashindano na mikutano mikubwa ya kimataifa vinaendelea kuongeza heshima ya nchi, huku akiweka bayana azma ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa moja ya vituo muhimu vya michezo barani Afrika.
“Tunaendelea kujenga msingi imara wa mafanikio ya muda mrefu katika sekta ya michezo,” amesema.



Comments
Post a Comment