RAIS wa Chama cha Wataalamu wa Milki Tanzania (AREPTA), Boniphace Yumba amesema madalali wasiosajiliwa wameendelea kuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi nchini.
Yumba amesema hali hiyo inatokana na baadhi ya watu kujihusisha na shughuli za udalali wa ardhi bila kuwa na usajili, taaluma wala kufuata taratibu rasmi za sekta hiyo.
Akizungumza leo Mei 14, 2026 katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Milki Tanzania (AREPTA), amesema sekta ya ardhi inahitaji usimamizi wa kitaalamu ili kulinda wananchi dhidi ya utapeli na hasara zisizo za lazima.
“Ni kweli kwamba kuna madalali ambao wanaharibu sana sekta ya ardhi. Sisi tuna wataalamu waliosajiliwa, wamesomea na wamebobea katika kazi hizi, lakini bado wapo watu wanaofanya kazi bila usajili na bila kufuata misingi ya kitaalamu,” amesema Yumba.
Kwa mujibu wa Yumba, wananchi wengi wanaolalamikia kupoteza fedha au kuingia kwenye migogoro ya ardhi wamekuwa wakifuata madalali wasiotambulika, jambo linalowafanya kukosa msaada wanapopatwa na matatizo.
“Tumekuwa tukiona watu wengi wakilia na kuilalamikia Serikali baada ya kutapeliwa, lakini mara nyingi matatizo hayo yanatokana na kutumia madalali ambao hawajasajiliwa,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuhakikisha wanapata ushauri kutoka kwa wataalamu wa milki, kampuni za real estate pamoja na ofisi za ardhi kabla ya kununua ardhi, nyumba au kufanya uwekezaji wowote.
“Ofisi za ardhi ziko wazi na zinatoa huduma nzuri. Wananchi waende kwa wataalamu waliosajiliwa kwa sababu hao wanawajibika kisheria na ni rahisi kusaidia changamoto zinapotokea,” amesema.




