WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete amesema hatua kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan zimeendelea kurejesha matumaini, furaha na ari mpya kwa watumishi wa umma nchini.
Kikwete aliyasema hayo wakati akizungumza na Maafisa Tawala pamoja na Maafisa Rasilimaliwatu katika mkutano uliofanyika katika Arusha International Conference Centre jijini Arusha, ambapo aliwataka viongozi hao kutekeleza wajibu wao kwa haki, weledi na kuwathamini watumishi wa umma ili waendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Nimewakumbusha kuleta furaha kwa watumishi wa umma ili nao waweze kupeleka furaha na neema kwa Watanzania,” amesema Kikwete.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya maamuzi makubwa yenye kugusa moja kwa moja maisha ya watumishi wa umma, hatua ambazo zimeonesha dhamira ya dhati ya kuboresha ustawi wao pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za serikali.
Kikwete ametaja uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali kupandisha madaraja watumishi 219,042 kuwa ni hatua ya kihistoria inayodhihirisha namna serikali ilivyojipanga kuimarisha sekta ya utumishi wa umma nchini.
Ameongeza kuwa hatua hiyo imekwenda sambamba na ongezeko la mishahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 mwaka 2025 pamoja na kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kwa asilimia 33.4 katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Kwa mujibu wa Kikwete, maboresho hayo yanagusa sekta nyingi muhimu ikiwemo afya, elimu, kilimo, mawasiliano, usafirishaji, nishati, viwanda, biashara, hoteli, michezo, uvuvi, bahari, madini na utamaduni.
Amesema takwimu hizo zinaonesha wazi kasi ya mageuzi ya kiutumishi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, huku zikithibitisha uongozi wenye maono unaoweka mbele ustawi wa watumishi, kuongeza morali ya kazi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.





Comments
Post a Comment