MBUNGE wa Jimbo la Kasulu Vijijini Edibilly Kazala amesema Tanzania inapaswa kuchukua hatua za haraka kuvilinda viwanda vya ndani na kukuza uwekezaji wenye tija, akionya kuwa sekta ya viwanda vya nguo nchini inaendelea kudorora kwa kasi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana Mei 22, 2026, Kazala amesema pamoja na ongezeko la wawekezaji wa kigeni nchini, bado kuna baadhi ya uwekezaji mdogo usio na manufaa makubwa kwa Taifa huku ukichukua nafasi ambazo Watanzania wana uwezo wa kuzifanya wenyewe.
“Lazima kama Taifa tuangalie namna ya kudhibiti baadhi ya uwekezaji usio na tija kubwa kwa wananchi wetu,” amesema.
Kazala amesema takwimu za ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa mwaka 2002 Tanzania ilikuwa na zaidi ya viwanda 50 vya nguo, lakini sasa vimebaki takribani vitatu pekee vinavyoendelea kufanya kazi, hali inayodhihirisha kuporomoka kwa sekta hiyo muhimu.
Amesema kushuka kwa sekta ya textile kumeathiri pia ajira, ambapo mwaka 2015 sekta hiyo ilikuwa imeajiri zaidi ya wafanyakazi 12,000 lakini mwaka 2016 idadi hiyo ilishuka hadi wafanyakazi 9,000.
“Tunazalisha pamba kwa wingi, lakini zaidi ya asilimia 80 ya pamba yetu tunaiuza nje kama malighafi badala ya kuongeza thamani hapa nchini kupitia viwanda vya ndani,” alieleza.
Mbali na sekta ya nguo, Kazala ameishauri Serikali kuongeza nguvu kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo (agro-processing industries), akisema sekta hiyo ni muhimu katika kujenga uchumi jumuishi na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sera na vivutio vya kodi vitakavyosaidia kuvilinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani kutoka bidhaa za nje.
“Utitiri wa kodi unaongeza gharama za uzalishaji na kufanya bidhaa zetu kushindwa kushindana kwenye soko la kimataifa,” amesema Kazala.


Comments
Post a Comment