Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi leo Mei 25, 2026 Bungeni Jijini Dodoma, Katambi amesema hadi kufikia Aprili 2026 jumla ya watuhumiwa 49,469 wa makosa ya kiuhamiaji walikamatwa, huku wahamiaji haramu 34,099 wakiondoshwa nchini baada ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika kuimarisha usalama wa mipaka, Katambi amesema Idara ya Uhamiaji imeanzisha Kanda Maalum za Uhamiaji katika mikoa ya Kagera na Kigoma kwa kuongeza askari pamoja na vitendea kazi ili kudhibiti wahamiaji haramu.
“Tutazidi kufanya misako, doria na kuanzisha kanda nyingine katika maeneo ya kimkakati yenye mwingiliano mkubwa wa wageni ili kuhakikisha wahamiaji haramu wanadhibitiwa ipasavyo,” amesema Katambi.
Aidha, amesema kampeni ya “Mjue Jirani Yako” imeendelea kuleta matokeo chanya baada ya wananchi kuongeza ushirikiano katika kutoa taarifa za wahamiaji haramu pamoja na kuelewa athari za kiusalama zinazotokana na uhamiaji usio halali.
Kwa mujibu wa Katambi,amesema kuanzia Julai 2025 hadi Aprili 2026 jumla ya vipindi 1,033 vya elimu vilifanyika kupitia redio, televisheni, shule pamoja na mitandao ya kijamii, hatua iliyosaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya uhamiaji na usalama wa taifa.
Sambamba na hayo, Katambi ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kushirikiana na Idara ya Uhamiaji kwa kuwafichua wageni wanaoishi katika maeneo yao kinyume na sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama,” amesema Katambi.
Katika hatua nyingine, Katambi amesema Serikali imeendelea kuboresha Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 68 zimetumika kununua vifaa vya TEHAMA, magari, malighafi za uchapaji wa pasipoti pamoja na ujenzi wa ofisi za uhamiaji.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imetenga Shilingi bilioni 69.94 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya, ununuzi wa magari 50 pamoja na vifaa vya TEHAMA kwa ofisi za uhamiaji zilizopo katika balozi za Tanzania nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha huduma za uhamiaji na usalama wa mipaka ya Tanzania.


Comments
Post a Comment