WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali itaendelea kuimarisha udhibiti wa changamoto ya “Lumbesa” ili kulinda wakulima, wafanyabiashara na walaji nchini.
Akizungumza leo Mei 22, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri Kapinga amesema Wakala wa Vipimo (WMA) una jukumu la kuhakikisha matumizi sahihi ya vipimo katika biashara kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura ya 340.
“Wizara kupitia WMA inaendelea kusimamia matumizi sahihi ya vipimo ili kulinda wakulima, wauzaji, wanunuzi na wasafirishaji wa mazao,” amesema Waziri Kapinga.
Ameeleza kuwa sheria hiyo inazuia mazao yaliyofungashwa kwa idadi au uzito kuzidi kilo 100, huku ikiruhusu kiwango cha ziada kisichozidi asilimia 5 (tolerance limit), pamoja na kuwajibisha wafanyabiashara kutumia mizani iliyohakikiwa angalau mara moja kwa mwaka.
“Sheria inaelekeza wazi kuwa vipimo lazima vizingatie viwango vilivyowekwa ili kuhakikisha haki inapatikana kwa pande zote,” ameongeza.
Aidha, Waziri Kapinga amesema Wizara imefanya operesheni tisa (9) katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Pwani, Morogoro, Mbeya, Iringa na Njombe.
Amesema katika operesheni hizo, magari 2,500 yalikaguliwa, ambapo 2,419 yalikutwa yakifuata viwango sahihi, huku 81 yakibainika kukiuka sheria na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kutozwa faini na kuamriwa kufungasha upya.
“Operesheni hizi zitaendelea nchi nzima ili kuhakikisha changamoto ya Lumbesa inatokomezwa,” amesema.
Pia, amesema Serikali imeweka vituo vya muda vya uhakiki wa vipimo katika ofisi za kata, mitaa na vijiji ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Aidha, baadhi ya Halmashauri za Mpanda, Kasulu na Kibondo zimetunga sheria ndogo zinazosisitiza matumizi ya mizani iliyohakikiwa na WMA katika biashara ya mazao.

Comments
Post a Comment