Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya ameendelea kuonyesha moyo wa kuendeleza vipaji vya vijana baada ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa Halmashauri ya Mji wa Bunda ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya UMITASHUMITA ngazi ya Mkoa wa Mara.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Mhe. Bulaya amesema dhamira yake ni kuhakikisha vijana wanapata mazingira mazuri ya kushiriki michezo na kuibua vipaji vitakavyowasaidia kufikia ndoto zao.
Aidha, ameahidi kutoa motisha kwa vijana watakaoshiriki mashindano hayo ili kuongeza ari ya ushindani na kuiwezesha Bunda kufanya vizuri katika UMITASHUMITA.
Mhe. Bulaya amekuwa mmoja wa wadau wakubwa wa michezo Mkoa wa Mara, ambapo kwa nyakati tofauti ameendelea kuisaidia timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Wilaya ya Bunda pamoja na shughuli mbalimbali za michezo kwa vijana.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Said Ramadhani, akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, alimpongeza Mbunge huyo kwa mchango wake mkubwa katika kuinua michezo na kusema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya michezo nchini








Comments
Post a Comment