WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho amesema Tanzania imeendelea kuwa salama huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiongeza nguvu katika kulinda mipaka ya nchi dhidi ya changamoto mbalimbali za kiusalama zinazojitokeza ndani na nje ya mipaka.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa leo Mei 19, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Dkt. Nyansaho amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 hali ya ulinzi na usalama katika mipaka yote ya Tanzania imeendelea kuwa shwari licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa ikiwemo uharibifu wa alama za mipaka, uchakavu wa barabara za ulinzi pamoja na migogoro ya ndani katika baadhi ya nchi jirani.
Amesema mipaka ya Tanzania yenye urefu wa kilomita 5,923.41 inayojumuisha nchi kavu, anga na eneo la maji imeendelea kulindwa kwa umakini mkubwa kupitia operesheni, doria na ushirikiano wa karibu kati ya JWTZ na vyombo vingine vya usalama.
Katika taarifa hiyo, Waziri huyo amesema mpaka wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeendelea kuwa salama licha ya athari za mapigano yanayoendelea Mashariki mwa DRC kati ya Jeshi la nchi hiyo na kundi la M23, huku JWTZ ikiendelea kufanya doria na kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hali ya usalama katika eneo hilo.
Aidha, amesema mpaka wa Tanzania na Msumbiji unaendelea kuimarishwa kutokana na uwepo wa kikundi cha kigaidi cha Ansar Al-Sunna Wal Jamaah (ASWJ) katika eneo la Cabo Delgado, huku Serikali ikiendelea kuongeza vifaa, zana na uwezo wa vikosi vya ulinzi kuhakikisha usalama wa wananchi na mipaka unaendelea kuimarika.
Dkt. Nyansaho pia amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za mipaka kwa njia za kidiplomasia, ikiwemo mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi pamoja na hoja ya mpaka kati ya Tanzania na Uganda.
Kwa upande wa usalama wa anga la juu, amesema Serikali imeendelea kujiimarisha kwa teknolojia, wataalam na mafunzo maalum ili kukabiliana na mabadiliko ya kiusalama yanayotokana na matumizi makubwa ya teknolojia za kisasa duniani.
Katika Bahari ya Hindi, amesema JWTZ kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama imeendelea kufanya doria za mara kwa mara kudhibiti vitendo vya uharamia, wahamiaji haramu, uvuvi haramu, biashara ya dawa za kulevya pamoja na matishio ya ugaidi.
“Lengo letu ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama wakati wote na wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu,” amesema Dkt. Nyansaho.















Comments
Post a Comment