MBUNGE wa Jimbo la Butiama, Wilson Charles Mahera ameipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua kubwa za mageuzi katika sekta ya elimu, akisema uwekezaji unaoendelea unalenga kuifanya Tanzania kuwa taifa la watu wenye ujuzi, ajira na uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia leo Mei 7, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Dkt. Mahera amesema mafanikio yanayoonekana sasa ni mwendelezo wa falsafa ya elimu ya kujitegemea iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Julius Nyerere mwaka 1967, ambayo inalenga kumjenga kijana mwenye ujuzi na mchango wa moja kwa moja kwenye uchumi.
Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia imeifanyia kazi changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuboresha sera ya elimu na mitaala, hatua inayolenga kuleta elimu yenye uhusiano wa moja kwa moja na soko la ajira.
“Kwa uongozi wa Dkt. Samia, tunaona mageuzi ya kweli kwenye elimu. Sasa elimu inazalisha ujuzi, si vyeti pekee,” alisema Dkt. Mahera.
Alimpongeza pia Waziri wa Elimu Adolf Mkenda kwa usimamizi wa utekelezaji wa sera mpya ya elimu pamoja na timu ya wataalamu wanaosimamia maboresho ya sekta hiyo.
Dkt. Mahera amesema Serikali tayari imejenga shule 103 za amali kwa zaidi ya shilingi bilioni 60 na shule nyingine 158 zinaendelea na mkondo wa elimu ya amali, hatua aliyoitaja kuwa ni msingi muhimu wa kuandaa vijana wenye ujuzi wa vitendo.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio hayo yatakamilika endapo Serikali itaongeza kasi ya uwekezaji katika Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), akieleza kuwa bado kuna upungufu wa fedha wa takribani shilingi bilioni 38.6 ili kukamilisha miradi hiyo muhimu.
“VETA ndiyo msingi wa ajira za kesho. Bila kuwekeza huko kwa nguvu, hatutafikia malengo ya ajira kwa vijana wetu,” amesema.
Sambamba na hayo Dkt. Mahera ameipongeza Serikali kwa kuanzisha programu za ufadhili wa masomo ndani na nje ya nchi pamoja na mfuko wa Samia Innovation Commercialization Fund unaolenga kukuza ubunifu na teknolojia kwa vijana.
Hata hivyo, ametoa wito kwa Serikali kuhakikisha fedha za maendeleo zinatolewa kwa wakati ili miradi yote ya elimu inayotekelezwa ikamilike bila kuchelewa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.


Comments
Post a Comment