_▪️Asema mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi_
_▪️Aonya tabia ya wagonjwa kupelekwa kununua dawa nje_
_▪️Asisitiza hospitali kutokuzuia miili ya marehemu kwa madai ya bili_
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote utaondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika kupata huduma za matibabu nchini.
Amesema hayo leo Jumamosi, Mei 16, 2026 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kondoa Mjini katika Uwanja wa Puma mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Waziri Mkuu amesema kupitia mfumo huo wananchi hawatalazimika tena kutumia gharama kubwa katika hatua mbalimbali za matibabu ikiwemo kumuona daktari, vipimo pamoja na ununuzi wa dawa.
“Kwa kuwa tunakwenda kwenye utaratibu wa Bima ya Afya kwa Wote, baadhi ya haya mambo yaliyokuwa yanawasumbua wananchi yataenda kupata jawabu la kudumu,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya nchini kupitia ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameonya vitendo vya baadhi ya hospitali kuwaelekeza wananchi kununua dawa nje wakati Serikali ikipeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa katika hospitali na vituo vya afya.
“Haiwezekani taarifa zioneshe utoshelevu wa dawa ni zaidi ya asilimia 90 halafu kila mwananchi akienda hospitali anaambiwa akanunue dawa nje. Hapo lazima pana mchezo mchafu,” amesema.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imeelekeza waganga wakuu pamoja na watendaji wanaosimamia ununuzi wa dawa kuhakikisha dawa zinazonunuliwa zinaendana na mahitaji ya wananchi katika maeneo husika.
“Nunuweni dawa kulingana na mahitaji ya eneo husika kwa sababu kila eneo lina aina ya dawa zinazotumika zaidi,” amesema.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za dawa katika maeneo mbalimbali ili kubaini kiasi cha fedha kilichotolewa, dawa zilizonunuliwa pamoja na matumizi yake.
“Nimetuma watu kufuatilia kila palipo na hospitali, fedha kiasi gani zimekwenda kwenye dawa, dawa kiasi gani zimenunuliwa na kiasi gani zimetumika,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Serikali yaliyopiga marufuku kuzuiwa kwa miili ya marehemu hospitalini kutokana na madai ya bili za matibabu.
“Tusizuie mwili kwa sababu yoyote ile. Waruhusu ndugu waendelee na taratibu za mazishi ya mpendwa wao,” amesema.





Comments
Post a Comment