RORYA.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mkoani Mara, Dk. Khalfan Haule, amesema serikali itachukua hatua za haraka za muda mfupi na muda mrefu kukabiliana na changamoto za Barabara, maji, afya na nishati ya umeme zinazoikabili kijiji cha Kwibuse iliyoko Kata ya Kisumwa wilayani humo
Dk. Haule ameyasema hayo baada ya kukagua uharibifu wa barabara ya Kuruya–Kwibuse–Marasibora, ambapo amesema kuwa sehemu ya barabara hiyo imekatika katika maeneo yenye makalavati matano mapya yaliyojengwa, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi na wasafiri.
Amesema hatua za muda mfupi zitahusisha kujaza mawe na vifusi katika maeneo yote yaliyoathirika ili magari na wananchi waweze kuendelea kutumia barabara hiyo, huku serikali ikiandaa mpango wa matengenezo makubwa zaidi ya kudumu.
“Mpango wa muda mrefu ni kunyanyua tuta la barabara hasa kwenye bonde la karibu na eneo la Kukona ili kuondoa kabisa tatizo hili,” alisema Dk. Haule alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kwibuse katika mkutano wa hadhara.
Katika sekta ya maji, Mkuu huyo wa Wilaya alisema mradi wa maji kutoka Komuge pamoja na visima viwili vilivyochimbwa umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mabomba unaofanywa na baadhi ya wananchi, hali inayosababisha maji kupotea kabla hayajawafikia wananchi.
Amesema serikali kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji imekubaliana kuimarisha ulinzi wa bomba hilo huku Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ukitarajiwa kufanya ukarabati wa maeneo yote yaliyoharibiwa ili huduma ya maji irejee katika hali ya kawaida.
Aidha, amebainisha kuwa serikali itanunua pump mpya ya kusukuma maji mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu ili kuwezesha kisima kilichochimbwa kufanya kazi kikamilifu hasa wakati wa kiangazi.
Kuhusu kisima cha Kukona, Dk. Haule ameliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta viongozi wa kitongoji wanaodaiwa kuhusika na wizi wa pump ya maji ili irejeshwe na huduma kuendelea.
Akizungumzia sekta ya afya, Dk. Haule ameeleza kuwa zahanati ya kijiji ina wahudumu watatu wa afya, lakini kwa sasa mmoja yupo masomoni, hivyo huduma zinaendelea kutolewa na wahudumu wawili waliobaki.
Amesema changamoto nyingine ni wahudumu hao kuishi katika kijiji jirani cha Nyanchabakenye, hali inayochelewesha wakati mwingine utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo, serikali imemwagiza mwenyekiti wa kijiji cha Kwibuse kuwatafutia wahudumu hao nyumba ya kupanga karibu na zahanati ili wawe karibu zaidi na eneo lao la kazi.
Pia amekitaka kijiji hicho kuendelea na ujenzi wa nyumba ya mganga ili ikikamilika iwe suluhisho la kudumu kwa makazi ya wahudumu wa afya. Aidha, ameahidi kuwa serikali itaipa kipaumbele zahanati ya Kwibuse mara itakapopata watumishi wapya wa afya ili kupunguza uhaba wa watumishi uliopo sasa.
Kwa mujibu wa Dk. Haule, licha ya changamoto zilizopo, zahanati hiyo inaendelea kutoa huduma huku ukarabati ukiendelea baada ya sehemu ya paa kuharibiwa na upepo ambapo Serikali tayari imetoa Sh milioni 3.7 kwa ajili ya kugharamia matengenezo hayo.
Kuhusu sekta ya elimu, Dk. Haule amesema wakati wa mkutano na wananchi hakuelezwa kuhusu uchakavu wa madarasa na uhaba wa madawati katika Shule ya Msingi Kwibuse, lakini ameahidi kufika binafsi kukagua hali hiyo wakati atakapokwenda tena eneo hilo kukagua maendeleo ya matengenezo ya barabara.
“Sijafika na wananchi hawakusema. Nikirudi kukagua matengenezo ya barabara nitapitia kuyaona,” alisema.
Aidha, alisema wananchi walimweleza kuhusu kubomoka kwa madarasa yaliyokuwa yakijengwa kwa nguvu na michango yao wenyewe, jambo lililomsukuma kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tatizo hilo na kuchukua hatua stahiki.
Kwa upande wa nishati ya umeme, alisema kati ya vitongoji sita vya kijiji hicho, vitatu tayari vina huduma ya umeme huku vitongoji viwili, ikiwemo Bosi, vikitarajiwa kupata huduma hiyo mwaka huu. Kitongoji kimoja kilichobaki kitapata huduma hiyo katika awamu inayofuata.
Dk. Haule alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha changamoto zote zinazogusa maisha yao zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.


Comments
Post a Comment