MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Marwa, ameibua kilio cha walimu wanaofundisha katika mazingira magumu vijijini huku akiitaka Serikali kuongeza walimu, kuboresha maslahi yao na kuwapa mazingira bora ya kazi ili kuinua kiwango cha elimu nchini.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia leo Mei 7, 2026 Bungeni Jijini Dodoma, Agnes alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kupitia ajira za walimu pamoja na utoaji wa ufadhili wa masomo ya juu ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa matumizi ya mifumo ya kisasa ya kidijitali ikiwemo School Information System, akisema mfumo huo umeongeza ufanisi katika kufuatilia taarifa za shule, walimu na wanafunzi nchini.
Hata hivyo, Agnes amesema bado kuna changamoto kubwa ya uhaba wa walimu katika maeneo mengi ya vijijini, hususan Mkoa wa Mara, jambo linalosababisha walimu wachache kubeba mzigo mkubwa wa wanafunzi.
“Walimu wetu wanapitia wakati mgumu sana. Wengine wanatembea umbali mrefu kwenda kufundisha, wanafika shule wakiwa wamechoka na wamejaa vumbi lakini bado wanaendelea kuhudumia watoto wetu kwa moyo mkubwa,” amesema.
Mbunge huyo ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia walimu wa vijijini usafiri wa uhakika, kuongeza hardship allowance pamoja na kushughulikia kwa wakati changamoto za mishahara, posho na kupandishwa madaraja.
“Walimu wanabeba maisha ya watoto wetu na mustakabali wa taifa hili. Wanahitaji kuthaminiwa na kupewa mazingira bora zaidi ya kazi,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Agnes ameibua suala la ukosefu wa ajira kwa vijana waliohitimu masomo ya biashara, akiiomba Serikali kuweka mkakati wa kuwajengea uwezo wa kujiajiri badala ya kusubiri ajira za Serikali pekee.
Amesema somo la biashara linapaswa kupewa uzito mkubwa kuanzia ngazi za chini za elimu ili kusaidia vijana kujenga uelewa wa kujitegemea kiuchumi mara wanapohitimu masomo yao.


Comments
Post a Comment