WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali imejipanga kutumia Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kuitangaza Tanzania kimataifa na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa taifa kupitia maboresho ya miundombinu, matangazo ya kimataifa na vifurushi maalum vya utalii.
Dkt. Kijaji amesema Tanzania ambayo ni miongoni mwa nchi tatu za Afrika Mashariki zitakazoandaa AFCON 2027, itanufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na mashindano hayo yanayotarajiwa kuvutia watazamaji wa viwanjani milioni 1.8 pamoja na watazamaji wa televisheni bilioni 1.9 duniani kote.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Mei 15, 2026 Bungeni jijini Dodoma, amesema Wizara imeandaa mkakati maalum wa kuitangaza Tanzania kabla, wakati na baada ya mashindano hayo.
Amesema kabla ya AFCON 2027, Tanzania itaanza kujitangaza katika Mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yatakayofanyika nchini Marekani kupitia mabango ya kidijitali pamoja na kushirikisha watangazaji maarufu wa michezo duniani kuitangaza nchi.
“Wizara pia itatumia watu maarufu na wenye ushawishi mkubwa duniani wakiwemo wanamichezo kutembelea vivutio vya utalii nchini na kurekodi maudhui yatakayorushwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo Instagram, TikTok, Facebook, LinkedIn na X,” amesema.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya utalii ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, mageti, malazi na njia za utalii katika maeneo mbalimbali hususan Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kuhakikisha wageni wanapata huduma bora wakati wote wa mashindano.
Ametaja baadhi ya maeneo yanayoendelea kuboreshwa kuwa ni barabara ya Seronera kuelekea Naabi, Ikoma na Lobo pamoja na huduma za malazi katika maeneo ya Sahare, Makuyuni, Wamimbiki na Pande.
Pia amesema Wizara itaunganisha Hifadhi ya Taifa Mikumi na reli ya kisasa ya SGR kupitia ujenzi wa lango la wageni eneo la Kilosa ili kurahisisha usafiri wa watalii watakaokuja kushuhudia AFCON jijini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa uwanja wa gofu wenye hadhi ya kimataifa katika Ikolojia ya Serengeti kwa lengo la kuvutia watalii wa michezo wakati wa AFCON 2027.
Kuhusu ubora wa huduma, amesema Wizara tayari imeanza kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya utalii ambapo waongoza watalii 2,228 wamepatiwa mafunzo maalum ya kuboresha huduma kwa wageni.
“Tutashirikiana na sekta binafsi kuandaa vifurushi maalum vya safari vitakavyounganisha utalii, usafiri, malazi na huduma nyingine muhimu kwa washiriki na mashabiki wa AFCON 2027,” amesema.
Dkt. Kijaji amesema mafanikio ya Tanzania kuendelea kuaminiwa kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kimataifa yanatokana na maono na diplomasia ya uchumi ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imeendelea kufungua fursa za uwekezaji, ajira na kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kudumisha ukarimu kwa wageni ili kuimarisha taswira ya Tanzania kama kivutio bora cha utalii duniani.











Comments
Post a Comment