Na: Dawati la Habari Polisi Mwanza
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu (Jinsia na Wanawake), Felista Mdemu, amewataka wanawake kuhakikisha harakati za kutafuta kipato hazivunji jukumu lao la msingi la malezi ya watoto katika familia.
Mdemu ametoa wito huo mkoani Mwanza April 25.2026 wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za "Mwanamke Kinara 2026" kwa Kanda ya Ziwa na Magharibi iliyofanyika katika Ukumbi wa Winter Fell City uliopo Nyasaka, Wilaya ya Ilemela.
Amesisitiza kuwa, pamoja na mwanamke kujiimarisha kiuchumi, ni muhimu kukumbuka kuwa malezi ya watoto ni sehemu ya wajibu wake wa msingi.
Katika hafla hiyo, jumla ya tuzo 17 zilitolewa, zikiwemo za Mwanamke Mpishi Kinara, Mwanamke Mapambo Kinara, Mwanamke Mwandishi wa Habari Kinara, Madini na Afisa Ustawi wa Jamii Kinara.
Katika kilele cha tukio hilo, Koplo, Stella Lyimo, ambaye ni Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana, alinyakua tuzo ya Mwanamke Kinara katika kipengele cha Ustawi wa Jamii ambapo alitajwa kufanya vizuri katika kutoa elimu ya kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa jamii.
Koplo Stella amewashinda washindani wake watano na kutajwa kuwa kinara namba moja kwa kuyafikia makundi mbalimbali ya kijamii na kuyapa elimu muhimu ya kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, hasa kwa wanawake na watoto.
Akizungumzia tuzo hiyo, Koplo Stella alitoa shukrani zake za dhati kwa waandaaji wa tuzo hizo kwa kutambua na kuamini kazi zinazofanywa na Jeshi la Polisi hususan kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto.
Mbali na kuwapongeza na kuwashukuru wale wote waliofanikisha ushindi wa tuzo hiyo, amesema tuzo hiyo ni chachu ya kuendelea kuitumikia jamii kwa weledi mkubwa.
Washindi wengine walionyakua tuzo ni Mapacha Catering Services ambaye ameshinda katika kipengele cha upishi wa chakula, Salma Mipawa ambaye ameshinda katika kipengele cha madini, na MC Phina ambaye ameshinda katika kipengele cha Mshereheshaji (MC) bora, ambao wote wamewashukuru waandaaji wa tuzo hiyo na Watanzania waliowapigia kura.
Zoezi hilo la utoaji tuzo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa; Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi; na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, SSP Virginia Sodoka, ambao, pamoja na mambo mengine, wamewakumbusha wanawake kuendelea kufanya kazi kwa umoja na mshikamano.
Tuzo za "Mwanamke Kinara" zilianza kutolewa mwaka 2021 ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuhamasisha wanawake katika harakati za kiuchumi na kijamii.







