Wananchi Chunya Kunufaika na Mradi wa Majiko Banifu kwa Bei ya Ruzuku.*

GEORGE MARATO TV
0

 





📌 *Majiko 1,555 kuuzwa kwa bei ya ruzuku* 

📌 *Serikali kutoa ruzuku ya asilimia 85 kwa kila jiko* .

📍 *Chunya, Mbeya* 

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa halmashauri hiyo, Wakili Athumani Bamba leo Aprili 24, 2026 amezindua rasmi mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku katika mji mdogo wa Makongolosi, wilayani Chunya mkoani Mbeya.


Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema mradi huo unalenga kuwapatia wananchi nishati mbadala iliyo nafuu, salama na rafiki kwa mazingira, huku ukichochea kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa ambao umeendelea kuwa chanzo cha uharibifu wa misitu.


Alieleza kuwa kupitia mpango huo wa ruzuku, wananchi wataweza kumudu kununua majiko banifu kwa gharama nafuu zaidi, jambo litakalosaidia kupunguza matumizi ya nishati zisizo rafiki pamoja na kuboresha afya za watumiaji kwa kupunguza athari za moshi majumbani.


“Ni muhimu wananchi wakautumia vyema mradi huu kwa kununua na kutumia majiko banifu, kwani yana manufaa makubwa kiafya, kiuchumi na kimazingira,” alisema.


Aidha, alibainisha kuwa halmashauri itaendelea kushirikiana na REA  kuhakikisha usambazaji wa majiko hayo unawafikia wananchi wengi zaidi katika kata na vijiji vya wilaya hiyo.


Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi kutoka REA, Ndugu Vencha Maganga  amesema gharama ya jiko moja ni Shilingi 50,580 lakini serikali imetoa ruzuku ya asilimia 85 sawa na Shilingi 42,993.00 kwa kila jiko na hivyo mwananchi atanunua jiko kwa bei ya Shilingi 7,587 akiwa ameambatanisha na kitambulisho cha taifa (NIDA).


Aidha, vituo vya uuzaji vimeandaliwa katika maeneo tofauti ili kurahisisha upatikanaji wa majiko hayo kwa wananchi wote.

 

Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo walieleza kufurahishwa na mradi huo, wakisema utasaidia kupunguza gharama za nishati ya kupikia pamoja na muda wanaotumia kutafuta kuni.


Mradi huo wa majiko banifu unatarajiwa kuwa mkombozi kwa kaya nyingi wilayani Chunya na kuchangia jitihada za kitaifa za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na endelevu.


 *Mwisho.*

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top