UMISSETA Nyamagana: Viongozi Wahimiza Amani, Nidhamu na Uadilifu

GEORGE MARATO TV
0

 

​Kutoka: Dawati la Habari Polisi Mwanza

Viongozi wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza wamewataka wanafunzi wanaoshiriki Mashindano ya Michezo kwa Shule za Sekondari (UMISSETA) ngazi ya wilaya, kuzingatia nidhamu, amani na uadilifu ili kupata wawakilishi bora watakaotetea ubingwa wa mkoa na taifa.

Wito huo umetolewa Aprili 27, 2026, wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Nsumba.

​Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Thomas Salala, aliwahimiza wasimamizi wa mashindano hayo kutenda haki wakati wa uteuzi wa washiriki.





Alisisitiza kuwa ni muhimu kupata vipaji halisi vitakavyoiwezesha Nyamagana na Mkoa wa Mwanza kuendelea kushikilia nafasi za juu katika ngazi ya mkoa na kitaifa. 

Sambamba na hilo, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Nyamagana, SSP Virginia Sodoka, aliwataka wanafunzi na washiriki wote kudumisha amani na utulivu muda wote wa mashindano hayo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

​Katika kuongeza msisitizo wa maadili, Afisa Elimu wa Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mwl. Deus Toga, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji, Kiomoni Kibamba, alisisitiza kuwa nidhamu ndiyo msingi mkuu wa mafanikio katika michezo na taaluma.

Afisa Michezo wa Halmashauri hiyo, Mohamed Bitegeko, alibainisha kuwa halmashauri imejiandaa vyema ili kuhakikisha wawakilishi watakaopatikana wana uwezo wa kutetea nafasi ya kwanza kitaifa katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 1, 2026.

Ili kuboresha zaidi viwango vya ushindani, Mratibu wa UMISSETA Wilaya ya Nyamagana, Mtesigwa Bulenga, aliiomba serikali kuendeleza miundombinu ya viwanja, kutoa mafunzo kwa walimu wa michezo, pamoja na kuongeza bajeti ya michezo hiyo kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

​Wakati wa hafla hiyo, Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana, Koplo Stella Lyimo, alitoa elimu kwa wanafunzi dhidi ya vitendo vya ukatili. Aliwataka washiriki kutovumilia ukatili wa aina yoyote na kuwahimiza kutoa taarifa mara moja kwa walimu au walezi wao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo.

​Mashindano hayo yanahusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mikono, kikapu, wavu, mpira wa meza, mpira wa kengele kwa wenye uono hafifu, riadha, sanaa za maonesho, pamoja na mashindano ya usafi na nidhamu.

Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: "Michezo na sanaa shuleni ni daraja la ajira na afya. Tushindane kimataifa kujenga heshima na kuinua uchumi wa Taifa letu imara."



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top