KAHAMA
Serikali kupitia Tume ya Madini imesema itaendelea kutoa bei elekezi za madini ya dhahabu, shaba na fedha kila siku itakayotumika kwenye masoko na vituo vya ununuzi wa madini hatua inayolenga kuongeza uwazi katika biashara ya madini na kuwawezesha wachimbaji kuuza madini yao kwa bei halisi ya soko la dunia.
Akifunga mafunzo kwa Mameneja na Wakaguzi Wakuu wa Migodi ya uchimbaji mdogo kutoka mikoa ya kimadini ya Kahama, Mbogwe na Shinyanga mapema jana, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, CPA Venance Kasiki alisema taarifa hizo za bei zitawasaidia wachimbaji kufanya maamuzi sahihi ya biashara na kuepuka hasara zitokanazo na madalali maarufu kama vishoka.
Alisema hapo awali baadhi ya wachimbaji walikuwa wakiuza madini bila kufahamu bei halisi ya soko la dunia, hali iliyosababisha kupoteza mapato na kuingia katika mikataba isiyo na manufaa.
Alifafanua kuwa kwa sasa bei za madini hutolewa kila siku, hivyo mchimbaji ana uwezo wa kufanya uamuzi sahihi kabla ya kuuza madini yake.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya uwazi katika biashara ya madini pamoja na kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya utoroshaji wa madini, ambapo watoa taarifa watapatiwa zawadi maalum.
CPA Kasiki alionya kuwa watakaobainika kujihusisha na utoroshaji wa madini watakabiliwa na hatua kali za kisheria ikiwemo kufunguliwa mashitaka, kutaifishwa madini, kulipa faini pamoja na kifungo kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama migodini, akibainisha kuwa uchimbaji usiofuata taratibu hauwezi kuwa endelevu, huku akisisitiza kuwa uhai wa binadamu una thamani kubwa kuliko madini.
Aliwahimiza wachimbaji kutumia maabara ya Tume ya Madini katika kupima sampuli ili kufanya maamuzi sahihi badala ya kutumia maabara zisizotambulika.
Aidha, aliwakumbusha wamiliki wa leseni kufanya miradi endelevu kwa jamii zinazozunguka migodi ikiwa ni utekelezaji wa takwa la Kisheria la wajibu wa mwenye leseni kwa jamii (CSR).
Awali, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando alisema mwitikio wa washiriki ulikuwa mkubwa ambapo kati ya washiriki 400 waliotarajiwa, washiriki 370 walijitokeza, jambo linaloonesha hamasa kubwa ya wachimbaji kujifunza masuala ya usalama, afya na utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SHIREMA, Hamza Tandiko alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa wa wachimbaji katika biashara ya madini, matumizi salama ya kemikali na baruti, uhifadhi wa mazingira pamoja na uchunguzi wa ajali migodini, akisisitiza umuhimu wa kuachana na uchimbaji wa kubahatisha na kuingia katika uchimbaji wa kisasa na wenye tija.




