JESHI la Polisi Mkoani, Tanga limefanikiwa kuzima mtandao wa utapeli wa kidijitali na kuwaokoa vijana 87 waliokuwa wamenaswa kwenye mtego wa biashara haramu ya upatu, huku likiwashikilia wasimamizi wawili wa kundi hilo kwa tuhuma za kujipatia mamilioni ya fedha kwa njia ya udanganyifu.
Operesheni hiyo kabambe iliyofanywa na Kikosi cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID), imefichua madudu ya kampuni inayojiita Champions E-Commerce Education, ambayo imekuwa ikitumia kivuli cha mafunzo ya biashara mtandaoni kuwarubuni vijana kutoa kiasi cha kuanzia Sh600,000 hadi Sh Milioni 4 kwa ahadi ya utajiri wa haraka.
Akithibitisha tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi, amesema vijana hao walikutwa wakiishi katika mazingira duni wakisubiri "utajiri hewa" huku watuhumiwa Mohammed Hamlima Idrisa (24) na Fidolini Hamisi Rashidi (21) wakiendelea kuratibu mkusanyiko huo haramu.
"Vijana hawa waliahidiwa faida kubwa ndani ya muda mfupi baada ya kutoa mamilioni hayo kama mtaji na gharama za mafunzo. Huu ni utapeli wa wazi unaolenga vijana wenye kiu ya maendeleo. Tunawashikilia wasimamizi hawa wawili na uchunguzi unaendelea ili kuwafikisha mahakamani," alisisitiza Kamanda Mchunguzi.
Tahadhari kwa Umma na 'Mitego' ya Kidijitali
Kamanda Mchunguzi ametoa onyo kali kwa wananchi wa Tanga na Tanzania kwa ujumla, kuwa makini na kampuni au taasisi zinazoahidi faida kubwa kwa muda mfupi bila kuwa na usajili wa mamlaka halali za kiserikali. Amesisitiza kuwa biashara yoyote inayomtaka mwanachama kuleta watu wengine ili apate faida (Pyramid Scheme) ni kinyume cha sheria na ni kiashiria tosha cha utapeli.
Tukio hili limeibua taharuki mkoani Tanga, likionyesha kuongezeka kwa mbinu mpya za kihalifu zinazotumia teknolojia (Cyber Fraud) kunyonya rasilimali za vijana. Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea na operesheni hiyo nchi nzima ili kusambaratisha mitandao yote inayofanya biashara za upatu kwa mgongo wa E-Commerce.
Mwisho


