Na: Mwandishi Wetu, Pangani
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Bara, Mussa Mwakitinya, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi wa mashindano ya mpira wa miguu wilayani Pangani yaliyopewa jina la Aweso Vijana Cup Aprili 4, 2026, katika uwanja wa mpira, Kata ya Mwera.
Mashindano hayo yamelenga kuongeza fursa ya ajira kwa vijana kupitia michezo, kuepuka magonjwa yasiyoambukiza, kujenga mahusiano na afya bora, huku Mbunge wa Jimbo la Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akiyafadhili mashindano hayo yaliyoandaliwa na Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM wilaya ya Pangani.
Pambano la uzinduzi litahusisha timu kutoka Kata za Mwera na Tungamaa. Akizungumza ofisini kwake Aprili 3, 2026, Katibu wa UVCCM wilaya ya Pangani, Nasri Mkalipa, amesema vijana wajiandae kikamilifu kushiriki mashindano hayo muhimu.
"Mbunge wetu Jumaa Aweso anawajali na kuwapenda vijana ndiyo maana amefadhili mashindano haya kwani siku hizi michezo sio burudani pekee lakini ni ajira pia, hivyo vijana tucheze kwa nguvu zote tukijua michezo ni kazi kamili," amesema Mkalipa.
Tayari Chama cha Mpira wa Miguu wilaya ya Pangani (PDFA), kimetoa kibali cha kufanyika mashindano hayo baada ya kupokea ombi la kuanziswa kwa mashindano hayo. PDFA wamesisitiza mashindano hayo yatumie waamuzi wenye vigezo, yazingatie kanuni 17 za mpira wa miguu bila kusahau zawadi kwa washindi.
Uwepo wa mashindano hayo ni utekelezaji wa ahadi za Aweso kipindi cha kuomba ridhaa ya Ubunge ambapo aliahidi kuanzisha ligi na kufadhili ligi mbalimbali wilayani humo ikiwa ni mkakati wake wa kusaka na kukuza vipaji vya vijana kupitia michezo kwa kuzingatia kuwa michezo ni ajira.



