Mradi wa umwagiliaji Bugwema wapewa msukumo mpya kukabidhiwa mkandarasi Aprili 18

GEORGE MARATO TV
0

MRADI Mkubwa wa umwagiliaji katika bonde la Bugwema, wilayani Musoma, katika halmashauri ya Musoma Vijijini mkoani Mara, umeanza kupata uhai mpya baada ya Serikali kuridhia kutolewa kwa shilingi bilioni 48 kwa ajili ya utekelezaji wake.

Hatua hii inalenga kuimarisha kilimo cha kisasa na kuinua uchumi wa wananchi wa eneo hilo.

Uamuzi huo umefikiwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuendeleza sekta ya kilimo na kupunguza umasikini kwa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 4, 2026 na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini, mradi huo unatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa mkandarasi, China Railway Bureau Ltd, Aprili 18, 2026 katika kijiji cha Bugwema, kata ya Bugwema kuanzia saa 4:00 asubuhi.


Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini, Sospeter Muhongo, ametajwa kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha kufufuliwa kwa mradi huo, baada ya kuupigania kwa muda mrefu tangu alipochaguliwa. Lengo lake kuu limekuwa ni kuwawezesha wananchi kutumia kikamilifu rasilimali za bonde la Bugwema pamoja na ukaribu wake na Ziwa Victoria kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mradi wa Bugwema una historia ndefu, ukiwa ulianzishwa mwaka 1974 na Hayati Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere, kabla ya kusimama kwa muda mrefu. Hata hivyo, juhudi za kuufufua zilipata nguvu mpya mwaka 2022 baada ya ombi la Mbunge huyo kupokelewa na kukubaliwa na Rais Samia, ambaye alielekeza Wizara ya Kilimo kuhakikisha unatekelezwa.

Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo katika mkoa wa Mara, kwa kuongeza uzalishaji wa mazao, kufungua fursa za ajira na kuinua kipato cha wananchi. Pia ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda unaotegemea kilimo imara na chenye tija.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top