MBUNGE wa Jimbo la Kondoa Mjini, Mariam Dittopile, ameitaka Serikali kufanya tathmini ya kina na kufungua mjadala mpana kuhusu uwezekano wa kuruhusu kilimo na biashara ya zao la mirungi Kwa mfumo rasmi wa kisheria.
Akichangia Bajeti ya wizara ya Kilimo leo April 29,2026 Bungeni Jijini Dodoma, Mhe.Mariam Dittopile amesema ni wakati sasa wa kuacha mtazamo wa kupiga marufuku bila uchambuzi wa kutosha, badala yake kuangalia fursa za kiuchumi zinazoweza kunufaisha Taifa.
Amesema kuwa nchi jirani zimekuwa zikivuna mapato makubwa kupitia zao hilo , huku Tanzania ikiwa haijatumia ipasavyo fursa iliyopo.
Aidha, Amesema Soko la mirungi lina mzunguko mkubwa wa fedha kimataifa, jambo linaloashiria uwepo wa chanzo kipya cha mapato iwapo kitawekewa mfumo sahihi wa usimamizi.
“Tunapaswa kujiuliza kama tunawanufaisha wengine bila sisi kujua. Wakati wenzetu wanakusanya mamilioni ya dola, sisi bado hatujachukua hatua ya kisheria kulisimamia zao hili,” amesema.
Ameishauri Serikali kuona umuhimu wa kufanya tafiti za kisayansi ili kubaini kwa uwazi athari za kiafya za zao hilo, akibainisha kuwa mjadala haupaswi kuongozwa na dhana bali ushahidi.
Aidha, alihoji ulinganisho wa madhara kati ya mirungi na bidhaa nyingine zinazotumika kihalali kama vile pombe kali na vinywaji vya kuongeza nguvu, akitaka kuwepo kwa mizani ya haki katika maamuzi ya kisera.
“Kama kuna madhara, tuyatazame kwa uhalisia na kulinganisha na vile vinavyoruhusiwa tayari. Tusifanye maamuzi kwa mazoea, bali kwa tafiti na takwimu,” ameongeza.
Ameishauri pia Serikali kuandaa miswada na kufanya utafiti wa kina kupitia taasisi husika, ili kubaini kama zao hilo linaweza kudhibitiwa kisheria na kuchangia ukuaji wa uchumi, ajira kwa vijana na mapato ya taifa bila kuhatarisha afya ya jamii.


