TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imebainisha kuwa magonjwa ya moyo yanaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya binadamu duniani, yakiongoza kwa kusababisha vifo zaidi kuliko magonjwa mengine.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma kuhusu Miradi ya Maendeleo na Fursa za Vijana kwa Mwaka 2025/26, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema kuwa takwimu zinaonesha hali ya kutia wasiwasi, ambapo kutokana na maradhi hayo yanayoweza kuzuilika kwa kiasi kikubwa iwapo hatua stahiki zitachukuliwa mapema.
Amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani watu milioni 17.9 hufariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa ya moyo, hali inayochangia karibu asilimia 75 ya vifo vinavyotokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.
Dkt. Kisenge amesisitiza kuwa mabadiliko ya mtindo wa maisha, ikiwa ni pamoja na lishe isiyo bora, ukosefu wa mazoezi, matumizi ya tumbaku pamoja na unywaji wa pombe, ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia ongezeko la magonjwa hayo.
"JKCI imeanza kutumia mifumo ya kisasa ikiwemo DOZEE inayowezesha ufuatiliaji wa wagonjwa kwa mbali pamoja na mfumo wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao, na hii tutawafikia wananchi Wengi kwa lengo la kuwapima na kuwapa ushauri endapo watagundulika kuwa na Magonjwa Mbalimbali ikiwemo Ugonjwa wa Moyo". Amesema
"wananchi wachukue hatua za kujikinga mapema kwa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuzingatia mtindo bora wa maisha". Ameongeza
Sambamba na Hayo amesema JKCI imeanzisha kampem Maalumu itwayo jua namba zako, yenye lengo la kumpima mtu ili ajue Afya yake na kupewa ushauri endapo atagundulika na ugonjwa wowote.
"Tukimpima mtu tutajua presha yake,tutajua mapigo ya moyo wake, mafuta yake mwilini, na tutamsaidia kumpa ushauri ili apunguze mathalani chumvi mwilini, vyakula vyenye chumvi, pamoja na mambo mengine". Amesema
JKCI imeendelea kuboresha huduma zake za matibabu ya moyo kwa kutumia teknolojia ya kisasa, hatua inayolenga kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kuokoa gharama kubwa kwa wananchi.








