WAZIRI wa Kilimo, Daniel Chongolo, amewasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2026/2027 leo Aprili 28, 2026, Bungeni jijini Dodoma ambapo amesema ni wakati kwa wawekezaji nchini kutumia fursa ya taka ozo kuzalisha mbolea hai, hatua itakayosaidia kuongeza tija kwenye kilimo sambamba na kulinda mazingira.
Akiwasilisha bajeti ya wizara yake Bungeni jijini Dodoma leo April 28,2026 Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo amezitaka halmashauri zote nchini kuiga mifano iliyopo kwa kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza mbolea hai kutokana na wingi wa taka zinazozalishwa.
"Ninatoa rai kwa Halmashauri nchini kuiga kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza mbolea hai kwa kutumia fursa ya taka ozo ambazo zinapatikana kwa wingi katika maeneo yao ikiwa na lengo pia la kusafisha na kutunza mazingira". Amesisitiza
"Kwa mfano Jiji la Dar Es Salaam kwenye dampo la Pugu, kwanza itasaidia kupunguza taka na kuzalisha mbolea hai". Ameongeza
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeongeza kasi ya kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji wa mbolea unaimarika, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima nchini.
"Serikali inalenga kumwezesha mkulima kupata pembejeo kwa urahisi na kwa gharama nafuu.Tunataka mkulima alime kwa tija na hilo linaanza na upatikanaji wa mbolea kwa wakati,”. Amesema
Hadi Machi 2026, zaidi ya tani milioni 1.25 za mbolea zimepatikana, huku tani zaidi ya 674,000 zikiwa tayari zimesambazwa kwa mfumo wa ruzuku kote nchini.
Hatua hiyo imeanza kuleta matokeo, ambapo matumizi ya mbolea yameongezeka na kuimarisha uzalishaji wa mazao.
Amesema Serikali pia imeimarisha Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na kuongeza uwezo wa usambazaji hadi vijijini, sambamba na uwekezaji kwenye uzalishaji wa ndani ili kupunguza utegemezi wa nje.
"Huu ni uwekezaji wa moja kwa moja kwa mkulima na uchumi wa taifa,” alisisitiza Chongolo.







