KATIKA mjadala unaozidi kushika kasi kuhusu mageuzi ya sekta ya kilimo, Mbunge wa Tarime, Mwita Waitara, ameibua hoja nzito akitaka Serikali kuanza kuangalia upya uwezekano wa kuruhusu kilimo cha bangi kama njia mbadala ya kuinua uchumi wa wakulima.
MBUNGE Waitara ameibua hoja hiyo leo April 29,2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati Akichangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo ambapo amesema kuwa tofauti na mazao mengi ya biashara, bangi ina gharama ndogo za uzalishaji kwani haihitaji matumizi makubwa ya mbolea wala pembejeo ghali.
Hali hii, kwa mujibu wake, inaweza kuwa mkombozi kwa wakulima wadogo wanaokumbwa na changamoto ya gharama kubwa za uzalishaji.
“Tunahitaji kufikiria nje ya mfumo wa kawaida. Kuna mazao yenye tija kubwa na gharama ndogo ambayo yanaweza kuwainua wakulima wetu,” ameeleza.
Mbali na mchango wake katika uchumi, Waitara ameangazia pia thamani ya bangi katika sekta ya afya, akibainisha kuwa imekuwa ikitumika katika matibabu ya baadhi ya magonjwa kama saratani na matatizo ya usingizi ikiashiria uwepo wa soko la kimataifa lenye ushindani.
Hata hivyo, hoja yake imekuja sambamba na kilio cha muda mrefu cha wakulima wa Tarime kukosa ukosefu wa masoko ya uhakika. Ameeleza kuwa wakulima wengi hujikuta wakipata hasara kutokana na bei duni au kunyanyaswa na wanunuzi, hali inayokatisha tamaa juhudi zao.



