Bajeti za Mashirika ya Umma kuchambuliwa kuakisi Dira 2050

GEORGE MARATO TV
0


Na Mwandishi wa OMH

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imeanza zoezi la uchambuzi wa mipango na bajeti za taasisi na mashirika ya umma, likilenga kuimarisha mchango wa taasisi hizo katika utekelezaji wa Dira 2050.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Alhamis, Aprili 2, 2026, Bw. Joseph Mwaisemba, Mkurugenzi Msaidizi wa Tathmini ya Mashirika yasiyo ya kibiashara (kwa upande wa mamlaka za udhibiti), alisema jumla ya watumishi 50 wa OMH wamekutana katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kuchambua bajeti za taasisi na mashirika ya umma 252.



Alisema uchambuzi huo unalenga kuangalia namna taasisi hizo zilivyojipanga katika kutekeleza Dira 2050 sambamba na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV).

“Tunachofanya hapa ni kuangalia kwa kina mipango ya taasisi na mashirika ya umma ili kuona namna inavyochangia utekelezaji wa Dira 2050 na mipango ya maendeleo ya taifa kwa ujumla,” alisema.

Aidha, alieleza kuwa zoezi hilo pia linahusisha uchambuzi wa mikakati ya taasisi hizo katika kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27.

Kwa mujibu wake, OMH inasimamia jumla ya taasisi 308, kati ya hizo 252 zinamilikiwa na serikali kwa hisa nyingi na 56 zinamilikiwa na serikali kwa hisa chache, huku jumla ya uwekezaji ukiwa ni Sh92.3 trilioni.

OMH pamoja na mashirika yake yaliyo chini yake yanatarajiwa kukusanya Sh1.8 trilioni kama mapato yasiyo ya kodi katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya bajeti ya Serikali inayokadiriwa kufikia Sh62 trilioni.

“Hivyo basi, unaweza kuona namna ambavyo zoezi hili lilivyo muhimu katika kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa,” alisisitiza.

Kisheria, utekelezaji wa zoezi hilo la uchambuzi unaongozwa na matakwa ya kifungu cha 10(2)(c) cha Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura ya 370, pamoja na kifungu cha 17(a) cha Sheria ya Bajeti, Sura ya 439, vinavyoitaka OMH kufanya uchambuzi wa mipango na bajeti za taasisi na mashirika ya umma yaliyo chini yake.

Kwa kuzingatia msingi huo wa kisheria, lengo la uchambuzi huo ni kuidhinisha mikakati na mipango ya mwaka ya taasisi na mashirika ya umma, na kuijumuisha katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa ajili ya usimamizi madhubuti wa utekelezaji pamoja na upatikanaji wa rasilimali za kugharamia mipango hiyo.

Aliongeza kuwa katika uchambuzi huo, wataalamu wanapitia mipango ya matumizi ya rasilimali kwa kuangalia mgawanyo kati ya matumizi ya kawaida, miradi ya maendeleo, pamoja na michango ya taasisi katika bajeti kuu ya Serikali.

Maeneo makuu yanayopewa kipaumbele ni pamoja na tathmini ya namna taasisi zilivyojipanga kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za Serikali na zile zinazotokana na vyanzo vya ndani vya mashirika husika.

Baada ya kukamilika kwa uchambuzi huo, bajeti zitaingizwa katika mfumo wa mipango na bajeti wa Serikali (PlanRep), kabla ya OMH kuendelea na jukumu la kufuatilia utekelezaji wake kwa kila robo mwaka ili kuhakikisha malengo yaliyokubaliwa yanafikiwa.

Bw. Mwaisemba alitoa wito kwa taasisi na mashirika ya umma kushirikiana kikamilifu katika kuhakikisha rasilimali chache zilizopo zinatumika kwa ufanisi katika upangaji na usimamizi wa mipango.

“Ufanisi wa kila shirika katika kutekeleza majukumu yake utaakisi moja kwa moja mafanikio ya utekelezaji wa Dira 2050 pamoja na mipango ya maendeleo ya taifa,” alisisitiza.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top