Waziri Mkuu Asitisha Ziara Kupisha Kumbukizi ya Miaka Mitano ya Hayati Dkt. Magufuli

GEORGE MARATO TV
0


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema ziara yake ya kikazi katika mikoa mbalimbali nchini itasimamishwa kwa muda kupisha kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, inayofanyika Machi 17, 2026.

Akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika Ikulu Ndogo ya Mpanda mkoani Katavi, Jumatatu Machi, 16, 2026 Waziri Mkuu alisema Serikali itaungana na Watanzania katika kumbukizi hizo za kitaifa za kumuenzi kiongozi huyo aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

 “Kesho hatutaendelea na ziara. Kama mnavyokumbuka ni siku muhimu kwa Watanzania wote, ikiwa ni kumbukizi ya miaka mitano ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa heshima hiyo kesho hatutakuwa na ziara,” amesema.

Amesema kumbukizi hizo zinafanyika kwa heshima ya kiongozi huyo aliyegusa maisha ya Watanzania wengi na kuacha historia kubwa katika uongozi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kusitishwa kwa ziara hiyo pia kutatoa fursa kwa viongozi wa mikoa na wilaya kushiriki katika vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vinavyopitia bajeti za wizara kabla ya kuwasilishwa rasmi bungeni.

Amesema katika hatua hiyo, wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa pamoja na wakurugenzi wa halmashauri wanatakiwa kushiriki moja kwa moja katika vikao vya kamati za Bunge kwa ajili ya kujibu hoja na kutoa ufafanuzi kuhusu bajeti za maeneo yao.

Vilevile, Waziri Mkuu amesema kipindi hicho pia kitatoa fursa kwa wananchi pamoja na watumishi kushiriki kikamilifu katika ibada na sherehe za sikukuu za kidini zinazotarajiwa kufanyika katika kipindi hiki.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itatumia kipindi hicho kufuatilia utekelezaji wa maelekezo na kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi wakati wa ziara yake katika mikoa iliyotembelewa.

“Tayari tumeshayasikia kutoka kwa wananchi, kuna yale ambayo tumeshayatatua lakini kuna yale ambayo yanahitaji ufuatiliaji zaidi wa kina,” amesema.

Amesema ratiba ya kuendelea kwa ziara hiyo katika mikoa mingine itatangazwa baada ya kukamilika kwa shughuli hizo za kitaifa na ratiba nyingine za kiserikali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top