MwanaFA ashuhudia mafundi wa soka Yanga

GEORGE MARATO TV
0


📍Aisifu GSM na Rais Hersi kwa kukuza vipaji vya watoto


Na Mashaka Mhando

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), amemwagia sifa Klabu ya Yanga na Taasisi ya GSM Foundation kwa jitihada zao za kuwekeza katika soka la vijana nchini, akisema hatua hiyo ni mustakabali wa mafanikio ya Taifa katika mchezo wa mpira wa miguu.

Mhe. Mwinjuma aliyasema hayo jana alipokuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa programu ya "Safari ya Soka" iliyoandaliwa na Klabu ya Yanga kwa kushirikiana na GSM Foundation, tukio lililofanyika katika viwanja vya Gymkhana Club, Dar es Salaam.

Akipokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, Naibu Waziri huyo alipata fursa ya kushuhudia vijana wadogo wakionyesha umahiri wao uwanjani, jambo ambalo alikiri kuwa limempa matumaini makubwa.

"Nimejionea mwenyewe, nchi hii ina 'mafundi' wa soka haswa. Vipaji vipo vingi sana, kinachohitajika ni uangalizi wa karibu na weledi kama huu unaofanywa hapa. Nina imani kubwa kuwa vijana 30 watakaopata nafasi ya kulipiwa na GSM Foundation kushiriki mafunzo haya, watakuja kulifaa Taifa letu huko mbeleni," alisema Mhe. Mwinjuma.

Aidha, MwanaFA alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa taasisi nyingine za sekta binafsi nchini kuiga mfano wa Yanga na GSM kwa kushirikiana na Serikali kuwekeza katika sekta ya michezo na burudani. Alisisitiza kuwa uwekezaji huo unaweza kuwa katika miundombinu au usimamizi wa vipaji ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi.

Kwa upande wake, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alimshukuru Naibu Waziri kwa kuunga mkono juhudi hizo na kubainisha kuwa klabu hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa inatengeneza misingi imara ya wachezaji watakaocheza soka la kulipwa ndani na nje ya nchi.

Programu hiyo ya "Safari ya Soka" inalenga kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya watoto kuanzia umri mdogo, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa Yanga katika kuimarisha kikosi chao cha vijana na kutoa mchango kwa timu za Taifa.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top