Dar es Salaam
Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) unatekeleza ujenzi wa barabara zenye urefu wa Kilomita 51.2 kwa kiwango cha lami na zege katika Kata zaidi ya nane (8) na mitaa isiyopungua 20 katika halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA wilaya ya Temeke, Mhandisi Paul Mhere ambapo ameeleza kuwa wameingia mikataba ya ujenzi wa barabara kwa gharama ya shilingi Bilioni 97.176.
"TARURA wilaya ya Temeke tuna mtandao wa barabara Kilomita 648.45, tuna majimbo matatu (3) ambayo ni Temeke, Chamazi na Mbagala na kote miradi inaendelea utekelezaji wake upo zaidi ya asilimia 75 isipokuwa Mbagala na Yombo mikataba ilisainiwa mwezi wa Aprili 2025 utekelezaji wake upo asilimia 32", amesema.
Ameongeza kuwa zaidi ya Kilomita 166 za barabara wilayani humo ni lami na zege, barabara za zege zinahimili uzito wa aina yoyote na zinadumu muda mrefu huku zikipunguza matengenezo ya mara kwa mara na kuondolea gharama serikali.
"Wilaya yetu ina bandari kavu na pia tuna bandari ambayo inahudumia nchi za Afrika Mashariki na Kati, hivyo malori yanayopita katika barabara zetu ni mengi, barabara hizi za zege zitadumu kwa muda mrefu na wananchi wameanza kufurahia maboresho ya miundombinu hii", amesema.
Naye, Diwani wa Kata ya Chang'ombe Mhe. Caroline Henrich amesema wamepata barabara sita (6) ambazo ni Igombe-Yemen, Songambele, Majimaji, Basra, Diwani na Mwakalinga ambapo hapo awali kipindi cha mvua maji yalijaa kwenye makazi ya watu na kusababisha kero lakini kukamilika kwa ujenzi wa mitaro sasa maji hayatuami na kero imeondoka pia thamani ya nyumba imepanda.
"Namshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu, awali barabara zilikuwa korofi Kata yetu ni mtambuka barabara kubwa ya VETA na ile inayoelekea Uwanja wa Taifa zikiwa zina foleni hakuna njia nyingine ya kupita zaidi ya barabara zetu, lakini sasa barabara zimejengwa imara kwa kiwango cha zege wageni wengi wanakuja kwa ajili ya biashara", amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Bora, Bw. Pius Kapungu ameeleza kuwa awali kulikuwa na mashimo na kipindi cha mvua maji yalikuwa yanaingia mpaka kwenye makazi ya watu lakini sasa wanashukuru mitaro iliyowekwa imesaidia hakuna maji na taa zikiwekwa kutakuwa salama mitaa itapendeza na ulinzi utaimarika.
Aidha, Bi. Saada Salim mkazi wa mtaa wa Majimaji ameipongeza serikali kwa ujenzi wa barabara na mifereji kwani kipindi cha mvua watu walishindwa kupata wateja wa kupangisha lakini sasa wanapata wateja wengi uchumi unakua, mazingira yamekuwa mazuri, maduka yamekuwa mengi na magari yanafika.
Naye, Bw. Jimmy Mwakipesile mkazi wa Chang'ombe maduka mawili amesema barabara imewarahisishia kusafirisha abiria kwa usalama tofauti na awali walikuwa wanadondoka kwenye maji na matope, pia sasa abiria wameongezeka kwa siku walikuwa wanapata shilingi 15,000 hadi 20,000 lakini sasa wanaweza kupata hadi shilingi 40,000 mpaka 50,000 kwa siku.







