Dkt.Mwigulu: wanafunzi watakaofaulu vizuri kusomeshwa na nchi kupitia Samia Scholarship

GEORGE MARATO TV
0




_Awafikishia wanafunzi salamu za Rais Dkt. Samia; asema Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu_

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema wanafunzi watakaofaulu kwa viwango vya juu watanufaika na ufadhili wa masomo kupitia mpango wa Samia Scholarship unaotolewa na Serikali.

Dkt. Mwigulu amesema hayo wakati akizungumza na wanafunzi katika ziara yake mkoani Rukwa, ambapo pia aliwasilisha salamu maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Daktari Samia Suluhu Hassan anasema kwa wale watakaofaulu kwa kiwango cha juu wanapata ufadhili asilimia 100. Na sio ufadhili tu wa asilimia 100 peke yake, asilimia 100 na unaenda kusoma nchi yoyote duniani… hiyo inaitwa Samia Scholarship,” alisema Waziri Mkuu.

Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu ambapo zaidi ya shule za sekondari 1,300, shule za msingi zaidi ya 2,700 pamoja na maelfu ya madarasa yamejengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Aliongeza kuwa Serikali pia imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu katika ngazi mbalimbali ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kufikia ndoto zao.

*AKAGUA UJENZI WA SHULE MILUNDIKWA*

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia alikagua ujenzi wa shule mpya ya Elimu ya Awali na Msingi inayojengwa katika eneo la Shule ya Sekondari Milundikwa wilayani Nkasi, mkoani Rukwa.

Mradi huo unagharimu shilingi milioni 329.5 zilizotolewa kupitia Programu ya Kuboresha Ubora wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST).

Ujenzi wa shule hiyo ulianza Oktoba 5, 2025 na unatarajiwa kukamilika Machi 20, 2026, ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 255 tayari zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa jengo la utawala, madarasa ya elimu ya awali, vyumba sita vya madarasa ya elimu ya msingi pamoja na vyoo kwa ajili ya wanafunzi na walimu.

Inatarajiwa kuwa kukamilika kwa shule hiyo kutaboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wa eneo hilo pamoja na kuongeza ubora wa elimu katika Wilaya ya Nkasi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top