Na mwandishi wetu Jovina Massano;Musoma.
Askofu wa Jimbo katoriki Musoma Michael Msonganzila awataka wanasiasa, waandishi wa habari na Jeshi la Polisi kuheshimu maeneo ya kanisa.
Ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari Machi 10,2026 Ofisini kwake huku akilaani vitendo vilivyotokea siku ya Ibada Machi 8,2026 na kuzua taharuki kwa waamini wa kanisa kuu la Jimbo katoriki Musoma.
Amesema ni vema Jeshi la Polisi likajenga mahusiano mazuri na jamii lakini pia amewataka wanasiasa kutofanya shughuli za kisiasa katika eneo la kanisa kwa kuwa vyama hivyo vina ofisi zao za kisiasa.
" Kanisa halikuwa na taarifa yeyote ya uwepo wa wanasiasa siku hiyo ya Ibada, bali kulikuwa na maombi ya kutumia eneo viwanja vya matumaini katika Vijana linalomilikiwa na kanisa katoriki baada ya kupata taarifa ya zuio kutoka Jeshi la Polisi kwa kuwa tuliwakubalia ilibidi tuwape taarifa ya kuwaeleza kuwa kwa kuwa hamna kibali Cha kufanya mikutano,na makongamano nchini,"amesema Msonganzila.
Ameendelea kusema kuwa kanisa haliruhusu mambo ya siasa kufanyika kanisani na kanisa halizuii mtu yeyote mwamini kushiriki Ibada hivyo Ibada iliendea lakini mara baada ya misa kuisha walei wa parokia wakaona wanawake wa BAWACHA wamekusanyika na kuanza kuongea na waandishi wa habari katika eneo la kanisa hivyo waliwataka waondoke waende kufanya mahojiano hayo maeneo yao.
Ameongeza kuwa katika mazingira haya waache kanisa liende na misingi ya utume wake, kanisa halijihusishi na siasa hivyo amewaomba wanasiasa kuacha kutochonganisha kanisa na taasisi nyingine kanisa lipo kwa ajili ya kujenga amani, mshikamano na kusimamia haki kwa jamii badala yake wakiwa wanahitaji kutoa ujumbe wowote watumie ofisi zao kwenye maeneo yao kutumia kanisa ni kutaka kuleta migogoro.
Aidha alaani Bawacha kufanya mahojiano na vyombo vya habari mbele ya eneo la Kanisa bila kibali cha kanisa.
Sanjari na hayo amewakumbusha waandishi wa habari kutumia taaluma yao vizuri bila kugonganisha Kanisa,Serikali au Chama chochote.
Atoa wito kwa waliohusika kuleta taharuki katika eneo la kanisa na kuleta changamoto kwa waamini kuwa na busara katika kuwasilisha ujumbe ndio hekima na huleta amani na mshikamano kwa jamii.


