Waziri Mkuu Aweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Hosteli Nelson Mandela

GEORGE MARATO TV
0


*Asifu maono ya Rais Dkt. Samia kuhimiza sayansi, atoa maagizo sita

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa wito kwa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Kampasi ya Tengeru ihakikishe inakuwa kitovu cha ubora wa kitaaluma na utafiti bunifu unaolenga kutatua changamoto halisi za dunia ya leo.

Ametoa wito huo leo (Jumapili, Februari 22, 2026) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Arusha, wanachuo na wakazi wanaoishi jirani na taasisi hiyo waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi katika hafla iliyofanyika kwenye Kampasi ya Tengeru, wilayani Arumeru, mkoani Arusha. 



“Tumeona tumeona chanjo ya samaki, tumeona mbolea inayozalishwa kwa kutumia mwani. Tumeona ndege nyuki ya kupanda mazao shambani, hii itaokoa muda wa unaotumika kupanda mazao. Hizi bunifu zote zinaundwa ili kurahisisha kazi kwani zinatatua mambo mengi kwenye shughuli za kila siku za maisha yetu,” amesema.

Aidha, ameitaka taasisi hiyo ihakikishe mafunzo yatakayotolewa, yanazingatia zaidi ujuzi wa vitendo, ubunifu na ujasiriamali ili wahitimu waweze kujiajiri, kuajiri wengine na kuwa sehemu ya suluhu ya changamoto ya ajira, badala ya kusubiri ajira serikalini pekee.



Ameutaka uongozi wa taasisi hiyo, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, uhakikishe matumizi ya TEHAMA, mifumo ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na usimamizi madhubuti wa rasilimali ili Kampasi hiyo iwe endelevu na shindani kimataifa.

Amewataka kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa jirani wakilinde na kukimiliki chuo kama rasilimali yao ya maendeleo kwa kushirikiana na Chuo katika kutoa huduma, mazingira rafiki na ushiriki wa kijamii.

Akisisitiza ukamilishaji wa hosteli hiyo, Waziri Mkuu amesema: “Kutokana na umuhimu wa hosteli hakikisheni hosteli hii inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaokusudiwa, na inaanza kutoa huduma ili matunda ya uwekezaji huu yaanze kuonekana mapema kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.”

Amesema ujenzi wa hosteli hiyo unaakisi dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza elimu ya juu na kuongeza nafasi za masomo katika nyanja ya sayansi kama nyenzo kuu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kuhusu upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuimarisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwa kuongeza bajeti yake kutoka sh. bilioni 464 mwaka 2020/2021 hadi sh. bilioni 916.7 mwaka 2025/2026, hatua ambayo amesema imewezesha vijana wengi zaidi kutoka familia za kipato cha chini kupata fursa ya kujiendeleza kielimu.

“Hatua hiyo imewezesha idadi ya wanufaika kuongezeka kutoka 177,925 mwaka 2021/2022 hadi 252,773 mwaka 2025/2026 sawa na ongezeko la asilimia 42.1. Sambamba na hilo, Serikali imeboresha mifumo ya utoaji mikopo kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa katika sayansi, teknolojia, uhandisi, tiba na sasa kilimo cha kisasa.”

Akimkaribisha kuzungumza na hadhira hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda alisema chuo hicho ni cha kipekee kwa sababu kinahusika na utoaji wa masomo ya sayansi na teknolojia tu na pia kinatoa shahada za Uzamili na Uzamivu tu.

“Chuo hicho kinakidhi maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kutoa ufadhili kamili kwa wanafunzi wanaofanya vizuri sana. Hawa Serikali inawalipia gharama zote kwa asilimia 100. Mheshimiwa Rais pia alielekeza tuwapeleke kusoma nje ya nchi vijana waliofanya vizuri sana.”

“Tulianza na vijana 50. Kati yao, vijana 16 walikuja hapa Nelson Mandela kupata mafunzo maalum na sasa wako Afrika Kusini. Hawa vijana 34 waliokuja awamu ya pili, wanapatiwa mafunzo na wao ikifika Septemba wataenda Ireland kuanza masomo yao,” alisema wakati akielezea mpango huo.

Mapema, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Balozi Maimuna Tarishi alisema ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika Kampasi ya Tengeru, unalenga kuongeza uwezo wa malazi wa wanafunzi kutoka 600 mwaka 2021 hadi 1,000 mwaka 2026. 

“Mradi unajumuisha jengo lenye ghorofa tatu katika mabawa matano ambalo lilikamilika litakuwa na vyumba 184. Kati ya hivyo, vyumba 160 ni self-contained, vyumba 20 ni  maalum kwa wanafunzi wa kike wenye watoto au mahitaji maalum na vinne vitakuwa kwa ajili ya matumizi mtambuka (common rooms).

Alisema mabawa matatu yako kwenye hatua ya umaliziaji na mawili yako kwenye hatua ya upauaji. “Ili kukamilisha ujenzi huu, zinahitajika sh. bilioni 1.88. Makadirio ya fedha hizo yako kwenye bajeti ya mwaka 2026/2027 na kama fedha yote itapatikana, tunatarajia ifikapo Desemba, 2026 majengo yote yatakuwa yamekamilika,” alisema.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top