DODOMA.
WAZIRI wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika Sayansi nchini ili kuendana na hitaji la Soko la Sayansi kwakuwa na Wanasayansi bora na wakutosha katika Sekta zote kutokana na kukua kwa teknolojia Ulimwenguni.
Profesa Mkenda ameyaeleza hayo leo Februari11 Jijini Dodoma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika sayansi Mwaka 2026.
Amesema takwimu zinaonesha wanawake wanasayansi duniani ni takribani asilimia 36 tu, hali inayoashiria kuwa bado kuna haja kubwa ya kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika sekta ya sayansi.
“Nchini Tanzania wanawake ni wengi kuliko wanaume. Kimsingi, tungewekeza vya kutosha katika kuwaendeleza wasichana kwenye masomo ya sayansi, tungekuwa na idadi kubwa zaidi ya wanasayansi wanawake,” amesema Waziri Mkenda.
Aidha,Prof. Mkenda amewataka wanafunzi, hususan wasichana, kujitokeza kwa wingi kusoma masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wataalamu na kuharakisha maendeleo ya taifa.
"uwekezaji katika sayansi una mchango mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya na teknolojia. Mfano wake ni maendeleo ya tiba nchini, ikiwemo huduma za upandikizaji figo katika hospitali za rufaa kama Hospitali ya Benjamin Mkapa. Mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji katika sayansi na teknolojia". Amesisitiza Prof. Mkenda
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia wanawake na makundi maalum,Mhandisi Mary Prisca Mahundi amesema kuwa kama Wizara Kazi yao kubwa ni kuhamasisha na kuwawezesha wanawake na wasicha kushiriki katika maendeleo ya sayansi kwakuboresha Sera pamoja na kusisitiza malezi bora.
“Kazi yetu ni kuhakikisha tunaboresha sera na miongozo inayowawezesha wasichana kupata fursa sawa katika elimu ya sayansi. Malezi bora ni pamoja na kumpa mtoto mwelekeo sahihi wa maisha yake ya baadaye,” amesisitiz Mhandisi Mahundi.
"Amewahimiza wasichana kujiamini na kuchagua masomo ya sayansi, akisisitiza kuwa hakuna kinachoshindikana kwa mtoto wa kike endapo atapata malezi na mazingira sahihi". Amehimiza
Serikali itaendelea kuweka mkazo katika masomo ya sayansi, ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaofanya vizuri ambapo wanafunzi watakaofaulu kwa kiwango cha juu masomo ya sayansi katika kidato cha sita watapata fursa ya kusomeshwa nje ya nchi kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended.















