▪️Ni kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mbunge na CRDB FOUNDATION
▪️Zaidi ya Wananchi 3000 kunufaika na mpango huu
▪️Mbunge Mavunde awataka wanamtumbu kuchangamkia fursa
▪️Mradi mkubwa wa kilimo upo njiani
Mbunge wa Jimbo la Mtumba Mh. Anthony Mavunde kwa kushirikiana ya CRDB BANK FOUNDATION kupitia programu ya Imbeju leo wameanza rasmi zoezi la kutoa mikopo ya Shiligi Bilioni 2 kwa ajili ya wajasiriamali wa Jimbo la Mtumba.
Akitoa taarifa ya awali, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB BANK FOUNDATION Bi. Tully Mwambapa amesema taasisi ya CRDB imejipanga kuhakikisha inawafikia wajasiriamali wengi nchini kwa lengo la kuwawezesha mikopo na mitaji ili kuendeleza shughuli za kiuchumi na kwamba Jimbo la Mtumba linakuwa ni moja kati ya majimbo ya mfano ambayo wajasiriamali zaidi ya 3000 kupitia vikundi vyao watapatiwa mikopo ya takribani Shilingi Bilioni 2.
Naye Mbunge Mavunde ameeleza dhamira ya mpango huu ni kuunga jitihada kubwa inayofanywa na serikali chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan ya kuwawezesha wajasiriamali nchini ukiwemo mkakati wa utoaji Shilingi Bilioni 200 kuchochea uchumi wa wananchi.
Aidha Mbunge Mavunde amewataka wananchi wa Mtumba kuchangamkia fursa nyingi zinazokuja za kiuchumi huku akigusia mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji ambao utafanyika Mtumba kwa kushirikiana na Mashirika makubwa ya Kilimo ya Bara la Afrika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mbunge wa Viti Maalum Mh. Dr Neema Majule,Mwenyekiti wa CCM Wilaya Cde. Charles Mamba na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mh. Alimon Chaula wamewataka wajasiriamali hao kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kunufaika na mikopo hiyo.








