*Asema yatahitajika madarasa 39,000 kukidhi mtaala mpya
*Akagua barabara ya Spencon - Mabogini -Kahe - Chekereni
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewaagiza watendaji wanaosimamia sekta ya elimu kuanzia sasa waanze kujenga shule zitakazokidhi mahitaji ya mtaala mpya wa elimu ifikapo mwaka 2028.
“Tulikuwa na vikao hivi karibuni, niliagiza ujenzi wa shule za sekondari nchini kuanzia sasa hivi uzingatie kuna madarasa 10 na shule zinapoenda kujengwa pawe na eneo la kutosha kujenga yote 10 au tuamue kujenga madarasa matatu kwenye yale saba yaliyokuwepo,” amesema.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Februari 20, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Mabogini mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Spencon - Mabogini - Kahe hadi Chekereni wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro. Alikuwa akijibu ombi la Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi ambaye aliomba kata hiyo ipatiwe sekondari.
Amesema mabadiliko ya mtaala wa elimu yanajumuisha miaka sita ya elimu ya msingi na miaka minne ya elimu ya sekondari. “Zamani tulizoea kusema kila kata iwe na shule ya sekondari lakini tuendako sasa itabidi kila kijiji kiwe na shule ya sekondari ili kumudu mahitaji hayo mapya.”
“Kama tuna bajeti ya kujenga majengo ya elimu, tuanze kuzingatia mitaala mipya. Kati ya mwaka 2026 na 2027, tunapaswa kuongeza madarasa 39,000 kwa maana kwamba tuna vijiji 13,000 na kila shule moja ya msingi itabidi iongezwe madarasa matatu.”
"Tunaposema kuanzia mwaka kesho, mwaka kesho wa bajeti hauko mbali. Ni miezi minne ijayo sababu mwaka mpya wa fedha unaanza Julai, mwaka huu. Na mwaka kesho, darasa la sita na la saba wataunganishwa na kufanya mtihani mmoja ili kujiandaa kuanza elimu ya lazima,” amesema.
Mapema, akielezea hoja kuhusu ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 31.25, Dkt. Mwigulu aliwaelekeza viongozi wa mkoa na wilaya wafuate utaratibu wa kuomba barabara hiyo ipandishwe hadi kutoka TARURA na kwenda TANROADS ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
RC na DC, TARURA na TANROADS fanyeni mchakato wa kuipandisha hadhi ya TANROADS ili ijengwe kw amara moja. Kwa muundo wake, barabara hii ni Bypass, kwa hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano katikati ya mji wa Moshi na pia itasaidia kutoa huku mazao ya wakulima.”
Barabara ya Spencon - Mabogini - Kahe hadi Chekereni inapita katikati ya vijiji 12 ambavyo ni Mabogini, Chekereni, Mtakuja, Oria, Miwaleni, Kahe, Mwangaria, Ngasini, Ngasini B, Soko, Kyomu na Gona.
Kwa mujibu wa taarifa ya ujenzi iliyosomwa mbele ya Waziri Mkuu, barabara hiyo ambayo itagharimu sh. bilioni 7.2, iko chini ya mtandao wa barabara wa TARURA Wilaya ya Moshi na inapita katika majimbo matatu ya Moshi Manispaa, Moshi Vijijini na Vunjo. Aidha, inapita katika kata tatu za Kahe Magharibi, Kahe Mashariki na Mabogini.
Ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kuimarisha shughuli za usafiri na usafirishaji na kuchochea uchumi kwenye maeneo yaliyo pembezoni mwa barabara hii kutokana na uwepo wa maeneo ya kilimo cha mpunga na mbogamboga.




