Na Angela Sebastian; Missenyi
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imefanya ziara katika kiwanda cha L and N Standerd Packaging Solution kilichopo Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera kinachomilikiwa na wawekezaji wazawa, kwa lengo la kuwatia moyo pamoja na kutoa elimu ya masuala ya uwekezaji na fursa zilizopo nchini.
Ziara hiyo iliyofanyika leo imelenga kuimarisha uelewa wa wamiliki wa viwanda kuhusu sera, taratibu na motisha zinazotolewa na serikali ili kukuza sekta ya viwanda na ajira kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa TISEZA Balozi Aziz Mlima amesema kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani ili waweze kupanua shughuli zao za uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Tupo hapa kuwatia moyo wawekezaji wazawa na kuwapatia elimu ya kina kuhusu fursa za uwekezaji, motisha zinazotolewa na Serikali pamoja na namna ya kunufaika na maeneo maalumu ya kiuchumi ili kukuza viwanda na ajira,” amesema Balozi Mlima.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa kiwanda cha L and N Standerd Packaging Solution Batreth Rwiguza ameeleza kuwa, kiwanda hicho kinazalisha vifungashio vya ukumbwa tofauti vikiwemo vya kilo 140 ambavyo vinatumika kubebea mazao na kuwa kiwanda kimeajiri watu 56 na kina thamani ya sh. Bilioni 6.




