Sido Mara na Ggf Yaja na Teknolijia ya Kuokoa Mitaji Kwa Wakulima wa Mbogamboga na Matunda

GEORGE MARATO TV
0


Na Mwandishi wetu Jovina Massano Musoma.

Shirika la viwanda vidogo vidogo (SIDO) mkoani Mara kwa kushirikiana na shirika la Grain to Grow Foundation (GGF) watoa mbinu ya kutumia Kaushio jua kwa wakulima wa mbogamboga na matunda ili kuokoa mitaji yao.

Akiongea na Mwandishi wetu meneja wa SIDO mkoani hapa Bi.Salome Mwasomola ameelezea namna bora ya kuongeza thamani  katika mazao ya mbogamboga na matunda kwa kusindika kupitia teknolojia ya nishati jua kwa kutumia kaushio hilo ambalo linaweza kukausha mazao hayo bila kuathiri viini lishe/ virutubisho vilivyomo.

Ameongeza kuwa teknolojia hiyo ni rahisi kutumiwa na wakulima kwa kuwa inatumia jua na inapatikana kwa urahisi  pia inaweza kutumiwa popote hata nyumbani.

Ifahamike kuwa utumiaji wa teknolojia hii ni njia mojawapo ya kuongeza thamani ya mazao  kwa wakulima na kuokoa mitaji ukizingatia  hata soko lake ni dogo kwa kuwa hakuna kiwanda cha kusindika mazao hayo mkoani hapa.

Amefafanua kuwa lengo utoaji elimu hii kwa wakulima  ni kuwezesha sambamba na kuijengea uwezo  jamii ya mkoa wa Mara kuweza kuhifadhi chakula chake nyumbani  na kuwezesha kupata mlo kamili na kuondoa hasara.

Tayari viongozi na wawakilishi 48 wa wakulima wa mazao hayo kutoka wilaya ya Rorya na Butiama wamepata mafunzo ya usindikaji ambayo SIDO na Shirika la  Grain Grow Foundation wameyatoa. 

Teknolojia hii ya kaushio jua ni rahisi kutumia na utengenezaji wake ni rahisi na ina uwezo wa kufyonza jua na kukausha bila kuharibu viini lishe vilivyomo.

Kaushio jua hilo  linapatikana katika Shirika la viwanda vidogovidogo(SIDO) pia mafunzo ya utengenezaji wake yanatolewa  katika shirika hilo.

Inafahamika kuwa tangu awali SIDO imekuwa  ni kituo cha taarifa kwa wajasiriamali na wanaohitaji kujiajiri kwa kuwa hutoa mafunzo ya kuwezesha kijana kujiajiri na kupata uwezo wa moja kwa moja kuanzisha viwanda vidogovidogo na vya kati.

" SIDO ina huduma nne ambazo ni uendelezaji wa teknolojia kwa kuwezesha upatikanaji wa mashine mbalimbali,pia mafunzo ya ujuzi na namna ya kuuza bidhaa zake,masoko kusaidia wajasiriamali kutangaza bidhaa ndani na nje ya nchi kupitia maonyesho mbalimbali huduma ya fedha inapatikana kwa ajili ya kuendeleza biashara na kuendesha viwanda vidogo na vya kati",amesema Salome.

Ni wakati kwa wakulima wa mazao hayo kutumia teknolojia ya Kaushio jua kwa kuwa ni suluhisho na mkombozi kwa kuokoa mazao hayo kuharibika na kuongeza thamani na kujiongezea vipato ambavyo vingepotea.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Grain Grow Foundation Amillen Saria amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na kupelekea majira kubadilika na uwepo wa athari za kimazingira  zinazopelekea wakulima kukumbwa na changamoto mbalimbali shirika limekuja na mpango mkakati wa kuokoa mitaji ya wakulima hao kwa kuwezesha ukaushaji wenye ubora zaidi.

"Shirika la GGF  limeazimia kusukuma suala la kilimo kutokana  na ukosefu wa wadau wa mazao yanayopewa kipaumbele na ukosefu wa soko kwa wakulima wa matunda na mbogamboga ", amesema Amillen.

Ameongeza kuwa SIDO akiwa ni mdau mkubwa katika uendelezaji na uwezeshaji wa upatikanaji wa teknolojia na masoko    inawezesha kwa kiasi kikubwa kuibua vyanzo vya ajira na viwanda vidogo kwa wajasiriamali hapa nchini.

Aidha ameongeza kuwa Ujengaji uwezo kwa vikundi vilivyolenga uzalishaji kupitia kilimo ni muhimu kwani inasaidia uboreshaji wa chakula katika kaya na kutambua umuhimu wa matumizi ya mboga hizo na matunda katika jamii.

Utoaji mafunzo umezingatia makundi ya wanawake na Vijana kuanzia miaka 18-45  katika Kata 12 na kufikia vikundi 58 vya wakulima,ufugaji, uzalishaji bustani  na chakula.

Aidha shirika la GGF hivi sasa limeanza  mradi unaolenga kutunza ardhi na mabadiliko ya tabia nchi ili kuwasaidia wakulima na kuhifadhi mazingira.

Usindikaji huu kwa kutumia Kaushio jua ni fursa kubwa kwa wajasiriamali kwa kuwa na uhakika kuepuka hasara katika mazao hayo.





               

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top