DODOMA.
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi la Tanzania kuwa na mazingira bora ya kazi ili liwe tayari wakati wote kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi pamoja na kulinda amani hali itakayo saidia kukuwa kwa uchumi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Februari 24, 2026, wakati akizindua jengo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa katika eneo la Kikombo, jijini Dodoma, ambapo ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo imekamilika kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 121, fedha zilizotolewa na serikali.
Kadhalika amesema kuwa dhamira ya kuliwekea mazingira bora Jeshi la Tanzania inatokana na dhana kwamba Taifa lolote linalotaka kuheshimiwa duniani halina budi kuwekeza katika taasisi imara za kulinda uhuru, mipaka, rasilimali na watu wake.
“Majengo haya mapya ni nyenzo tu za kutekeleza majukumu yetu, lakini nguvu ya jeshi haitokani na majengo wala vifaa peke yake,” amesema Rais Samia.
Akitoa ufafanua wa gharama za mradi huo Katibu mkuu wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe amesema zaidi ya Bilion 318 zimetumika katika ujenzi wa Majengo ya makao makuu ya ulinzi wa taifa kwa awamu ya kwanza huku fedha zote zikitolewa na serikali.
"Namshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani na Serikali yake Kwa ujumla kwa kutoa fedha hizo kwani imerahisha mradio huo kukamilika kwa wakati". Amesema
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, amesema shilingi bilioni 121 zimetumika kukamilisha ujenzi wa jengo kuu, majengo saidizi, miundombinu ya kuunga mkono, pamoja na ununuzi wa samani zote za ndani za Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa yaliyopo Kikombo, jijini Dodoma.
"Fedha zote hizo zimetolewa na Serikali kwa lengo la kukamilisha ujenzi wa makao makuu hayo, ambayo yanajumuisha ofisi za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na ofisi zote za Makao Makuu ya Jeshi". Amesema
“Makao Makuu haya ya kudumu ya ulinzi wa taifa ni ya kwanza kabisa kihistoria katika jeshi letu. Kama wote mnavyojua, kabla ya makao makuu haya, jeshi lilikuwa na makao makuu yake Upanga, Dar es Salaam, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964,” ameongeza Jenerali Mkunda.
"Lakini pia tunakushukuru Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huu hali ambayo imeleta morali na heshima kwa jeshi nchini". Amesisitiza
Mradi wa ujenzi wa Makao makuu ya ya ulinzi wa taifa kwa awamu ya kwanza umekamilika katika Kata ya Kikombo Jijini Dodoma huku jengo hilo likihusisha ofisi zote za wizara ya ulinzi.















