Ppra Yatoa Mafunzo ya Mfumo wa Nest Kwa Makundi Maalum Wilayani Musoma

GEORGE MARATO TV
0


Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Ziwa, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, hii leo imeendesha mafunzo maalumu kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na makundi maalumu kuhusu namna ya kujiunga na Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kielektroniki (NeST) na fursa zinazopatikana kupitia mfumo huo katika ununuzi wa umma.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu ambao ni raia wa Tanzania ili waweze kushiriki kikamilifu katika zabuni za Serikali kupitia mfumo wa NeST, sambamba na utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni zake za mwaka 2024 zinazozitaka taasisi nunuzi kutenga asilimia 30 ya thamani ya ununuzi wao wa mwaka kwa makundi maalumu.

Kupitia mfumo wa NeST, makundi maalumu yatapata fursa ya kushiriki katika zabuni mbalimbali za Serikali ikiwemo huduma za ujenzi, usafi wa mazingira, ulinzi na usalama kazini pamoja na huduma zinazohitaji ujuzi, teknolojia na uzoefu, fursa hizi zinalenga kuwawezesha kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya jamii.

Akitoa mafunzo hayo kwa niaba ya PPRA Kanda ya Ziwa, Bw. Emmanuel Mgini na Bi. Ghati Chacha ambao ni maafisa kutoka PPRA, wameeleza kuwa mfumo wa NeST umeanzishwa ili kuongeza uwazi, ushindani na ufanisi katika mchakato wa ununuzi wa umma huku wakisisitiza umuhimu wa makundi maalumu kutumia fursa zinazotengwa kwao na kuhakikisha wanazingatia masharti yote ya usajili.

 













Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Manunuzi na Ugavi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Bw. Idd Mohamed Buruna, amewahimiza wananchi wa makundi maalumu kuunda vikundi na kujisajili katika mfumo wa NeST ili kunufaika na asilimia 30 ya zabuni zinazotengwa kwa makundi hayo kila mwaka kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.

Nae Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Bw. Alade Maluli, amesisitiza kuwa fursa hiyo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha makundi maalumu yanapewa kipaumbele katika shughuli za maendeleo, hivyo amewataka wananchi kutumia kikamilifu mfumo wa NeST ili kuongeza ushiriki wao katika ununuzi wa umma.

 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top